Sunday, August 18, 2024

RC Dendego Amshukuru Rais Samia kwa Miradi ya Maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego, ametoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa za maendeleo zinazotekelezwa mkoani humo.

Akizungumza na wananchi katika Kata ya Iguguno Wilayani Mkalama (Agosti 18, 2024) kwenye ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  Zubeir Ali Maulid, iliyolenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, Dendego ameeleza kuwa Serikali chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,  imefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa kila sekta, ikiwemo kilimo, miundombinu ya elimu, maji, afya, uwekezaji, nishati ya umeme, barabara ambayo imeleta mafanikio makubwa kwa wananchi wa Singida.

Akizungumza kuhusu sekta ya kilimo, Mheshimiwa Dendego amesema kuwa mkoa huo umefanikiwa kuzalisha chakula cha kutosha kutokana na uwekezaji mkubwa kwenye skimu za umwagiliaji.

 "Licha ya changamoto ya mvua kuwa ya kiasi, kupitia skimu hizi za umwagiliaji, tumefanikiwa kupata chakula cha kutosha na tumefuta kabisa tabia ya kuomba msaada wa chakula," alisema Dendego.

Mkoa wa Singida unajivunia kuwa na skimu za umwagiliaji zipatazo 24 ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa  alibainisha kuwa wamefanikiwa kupata mbegu bora na ruzuku ya mbegu, hali iliyowezesha kuzalisha zaidi ya tani tisa za chakula.

Kwa hatua hizi za maendeleo, RC Dendego amemshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake makini na uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo na nyinginezo, ambazo zimeleta tija kwa wakulima na wananchi wa Singida kwa ujumla.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha mkoa huo unazidi kupiga hatua kubwa zaidi katika maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akizungumza na wananchi wa Kata ya Iguguno Wilayani Mkalama kwenye ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid iliyohusu kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024

Baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo uliofanyika katika Kata ya Iguguno Wilayani Mkalama kwenye ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid iliyohusu kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 



No comments:

Post a Comment