Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka wahudumu wa afya mkoani Singida kuzingatia maadili, utu na kuwajali wananchi wanapotoa huduma za afya, akisisitiza kuwa mteja ndiye mhimili mkuu wa mafanikio ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote. Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) mkoani Singida.
Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha waganga wafawidhi wa vituo vya afya mkoa wa Singida, Dkt. Mganga amesema Serikali inaanza utekelezaji wa bima hiyo kwa majaribio kwa makundi maalum, hivyo ni muhimu wahudumu wa afya kuwahudumia wananchi kwa weledi ili kila mmoja anufaike na mpango huo. Amesema huduma duni au lugha isiyofaa inaweza kuwakatisha tamaa wananchi na kudhoofisha lengo la Serikali la kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wote.
Dkt. Mganga amewataka pia wasimamizi wa huduma za afya kufanya marekebisho na kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya afya ili wananchi wasijutie kujiunga na mfuko wa bima ya afya, hususan kwa makundi maalum ambayo Serikali itayalipia gharama. Amesisitiza kuwa mazingira ya vituo vya afya yanapaswa kuboreshwa ili mwananchi anapofika ajisikie kuthaminiwa na kupata huduma stahiki.
Aidha, amezitaka taasisi za afya kuhakikisha zinalipa madeni yanayodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) kwa wakati, ili kuwezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na huduma muhimu zinazokidhi mahitaji ya wananchi. Amesema upatikanaji wa dawa na vifaa ni msingi wa utoaji huduma bora na mafanikio ya bima ya afya kwa wote.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida amewataka wahudumu wa afya kuvaa mavazi rasmi yanayotambulika ili kuongeza uaminifu kwa wagonjwa na kuimarisha taswira ya sekta ya afya. Ameongeza kuwa matumizi ya lugha nzuri na yenye staha kwa wagonjwa ni msingi muhimu wa kudumisha uhusiano mzuri kati ya wahudumu wa afya na wananchi.
Kwa niaba ya waganga wafawidhi wote wa mkoa wa Singida, viongozi wa vituo vya afya wameahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa kwa kuboresha huduma za afya, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha vituo vinaingiza mapato yatakayosaidia kuendeleza huduma. Wamesema dhamira yao ni kuufanya Mkoa wa Singida kuwa mfano wa utoaji huduma bora za afya nchini Tanzania.
Kikao kazi hicho pia kimewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wakiwemo wawakilishi wa NHIF, TIRA, MSD na taasisi nyingine, ambao waliwasilisha mada na maelezo kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayotarajiwa kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya kwa wananchi wote.






No comments:
Post a Comment