Friday, August 18, 2017

KUMBUKUMBU NZURI YA IGP SIRRO NA WAANDISHI WA HABARI SINGIDA.

Mwandishi wa Habari wa ITV/Radio One Mkoa wa Singida Elisante Mkumbo akifurahia wakati akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya Polisi Nchini IGP Simon Sirro.
 
Mwandishi wa Habari wa Startv/Radio Free Africa Mkoa wa Singida Emmanuel Michael akifurahia wakati akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya Polisi Nchini IGP Simon Sirro.
 
Mwandishi wa Habari wa Habarileo/Daily News Mkoa wa Singida Abby Nkungu akifurahia wakati akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya Polisi Nchini IGP Simon Sirro.

Monday, August 14, 2017

“TUMEPATA UHAKIKA WA MBEGU BORA YA ALIZETI, MBEGU FEKI ZILITUKATISHA TAMAA”, WAKULIMA WA ALIZETI SINGIDA.


Mwenyekiti wa chama cha Wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima akisisitiza jambo katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.
 

Meneja wa Mradi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya akiandika maoni ya wakulima wa alizeti wakati wa majadiliano katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti.


Baadhi ya wakulima wa alizeti wakiandika baadhi ya maelekezo, mapendekezo na maoni yaliyotolewa katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.

Wakulima wa zao la alizeti Mkoani Singida wamepata uhakika wa mbegu bora ya alizeti ambayo itawasaidia kuzalisha kibiashara tofauti na hapo awali walipokuwa wakipata mbegu zisiso na uhakika wa mavuno mazuri.

Mwenyekiti wa chama cha Wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima amesema hayo mapema leo katika mkutano wa wadau wa kilimo cha alizeti ulioandaliwa na mradi wa Faida Mali kupitia Shirika la AMDT ambalo limejikita katika kusaidia wakulima wa zao hilo kupata mbegu bora.

Sima amesema hapo awali wakulima walikuwa wakinunua mbegu kwa wauzaji ambao sio waaminifu na hivyo kutovuna vizuri kutokana na mbegu hizo kuota vibaya na kutoa alizeti kidogo.

Amesema mradi wa Faida Mali umewahakikishia kuwasaidia upatikanaji wa mbegu bora na ya kisasa na hivyo kukifanya kilimo cha alizeti kuwa kama biashara nyingine ambazo zina faida kubwa.

“Hawa Faida Mali sisi tunawaamini kwakuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali hivyo watatusaidia katika kupata mbegu bora, tulikuwa tunaumizwa na wauzaji wengine akikuuzia mbegu inaota hapa, pale haioti matokeo yake unapata hasara” amesema na kuongeza kuwa,

“Mkulima akipata Mbegu bora hiyo ni hatua ya kwanza ya mafanikio, kwakweli baadhi yetu tulianza kukata tamaa kwa kuona tunapata hasara tu, unalima alizeti miaka mingi huoni faida kubwa kama ambavyo unatarajia, lakini mradi huu umetuonyesha njia ya mafanikio, nawaomba wakulima wengine waweze kujiunga katika vikundi ili waweze kufikiwa na mradi huu au miradi mingine”, amesisitiza.

Naye Mkulima wa alizeti Kutoka kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida amesema utaratibu wa kununua alizeti kwa magunia ya lumbesa badala ya vipimo vya mizani unawapunja wakulima na kuwafanya warudi nyuma kiuchumi.

Laida amesema wanunuzi wa alizeti wanapakia alizeti katika magunia na kushindilia ambapo kipimo hicho sio sahihi na hakilengi kumwinua mkulima hivyo basi mradi wa Faida Mali unapowasaidia kutafuta masoko uangalie na vipimo vinavyotumika katika kununua zao hilo.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya amesema ili wakulima wazalishe kibiashara watawasaidia kupata mbegu bora na ya kisasa, kupata huduma mbalimbali za ugani, masoko na kuwaunganisha wakulima hao na huduma za kifedha.
 
Mkondya amesema kwa kushirikia na Autainsurance watawasaidia wakulima kupata elimu ya faida za bima na hivyo watakata bima ya mazao yao ili wakipata majanga yoyote kama vile moto, mafuriko, au mbegu kutoota wataweza kufidiwa na kuepuka hasara.

Ameongeza kuwa kupitia watoa huduma wao ambao ni Ersoko wamejipanga kutoa elimu kwa wakulima hasa kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno ambapo mkulima atapata taariza zote za kilimo cha alizeti kulingana na eneo alipo kwa kumuelekeza mbinu za kulima kisasa, muda wa kupanda, aina ya mbolea na taarifa za masoko ya mazao yake.

Mkulima wa alizeti Kutoka kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida akifafanua jambo katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.


Mkurugenzi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Tom Silayo akiwaelezea wakulima wa alizeti mambo ambayo mradi huo utayatekeleza. 


Afisa Kilimo Sekretarieti ya Mkoa wa Singida Mashaka Mlangi na Afisa Maendeleo ya Jamii Patrick Kassango wakichukua maoni ya wakulima walioudhuria kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.

Sunday, August 13, 2017

AJALI ZAPUNGUA MKOANI SINGIDA, JESHI LA POLISI LAWEKA MIKAKATI KUPUNGUZA ZAIDI AJALI NA UHALIFU.Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ACP,Debora Daud Magiligimba, akitoa taarifa juu ofisini kwake.


Jeshi la Polisi Mkoani Singida, limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kutoka ajali 69 kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi kufikia ajali 24 katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Juni mwaka huu.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ACP Debora Magilingimba wakati akitoa taarifa ya uhalifu kwa Mkoa wa Singida ambapo amesema katika ajali hizo 24 zilisababisha vifo vya watu 29 na hapajakuwepo majeruhi kabisa.
 
ACP Magiligimba amesema kupungua kwa ajali kumetokana na Jeshi hilo kutoa elimu ya usalama barabarani mara kwa mara hasa katika maeneo ya vijijini, mitaani na hata katika mafunzo ya udereva.
 
Ameongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likithibiti mwendo kasi katika barabara kuu, kuthibiti ulevi kwa upimaji wa kilevi kwa madereva wote wa vyombo vya usafiri na hivyo kupelekea ajali kupungua sana kwa Mkoa wa Singida.
 
“Pia tumeendelea kutoa elimu ya usalama barabarani mashuleni, vyuoni na katika  nyumba za ibada. Lengo ni kuiongozea jamii uelewa zaidi unaohusu masuala yote ya ulinzi na usalama, na sheria za usalama barabarani”, amefafanua.
 
Aidha, ACP Magiligimba amesema makosa madogo yamepungua kwa asilimia 0.8 ambapo jumla ya makosa madogo 22,222 yameripotiwa katika kipindi cha januari hadi juni mwaka huu, ikilinganishwa na makosa kama hayo 22,403 yaliyotokea kipindi kama hicho mwaka jana.
 
“Katika makosa hayo madogo, jumla ya wakosaji 21,836 walilipa faini mbalimbali zaidi ya shilingi milioni 655. Katika kipindi kama hicho mwaka jana jumla ya wakosaji 21,778 walilipa faini mbalimbali zaidi ya shilingi milioni 653.3. Faini hizo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.3”, amesema kamanda huyo.

ACP Magiligimba ametaja baadhi ya mikakati mbalimbali ya kukabiliana/kupunguza zaidi uhalifu, wahalifu na ajali za barabarani kuwa ni kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia vyombo vya habari na kushirikiana na asasi mbalimbali katika kutoa elimu na matengenezo ya barabara.
 
“Vile vile tutaendelea kuimarisha ushirikiano zaidi na asasi zisizo za kiserikali, ikiwemo World Future Vocation, mabalozi wa usalama barabarani na SUMATRA. Pia tutashirikiana na TANROADS, halmashauri za wilaya na manispaa kushauriana namna ya kufanya matengenezo ya barabara katika maeneo yaliyoharibiwa au yenye kusababisha ajali za mara kwa mara”, amesema ACP Magiligimba. 

Picha/habari na Nathaniel Limu.