Monday, April 22, 2024

MKOA WA SINGIDA WAANZA KUTOA CHANJO YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI KWA WASICHANA 178,114.

Mkoa wa Singida umezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo wa Saratani la mlango wa kizazi kwa wasichana mwenye umri kati ya miaka Tisa (9) hadi 14 ambapo Wasichana 178, 114 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo mkoani humo.

Akizindua zoezi la utoaji wa Chanjo hiyo katika Kijiji cha Kisaki Manispaa ya Singida, Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego (leo 22-Aprili-2024 ) amewaagiza Maafisa Afya wahakikishe maeneo yote yaliyoandaliwa kutolewa huduma hiyo ya chanjo yanafanya hivyo kwa viwango vya juu ili kuwalinda watoto wa kike na saratani hiyo hatari.

Dendego amesisitiza kuwa chanjo hiyo pia ni lazima iwafikie wanafunzi wanaosoma kwenye shule binafsi na watoto wa kike ambao wanaishi mitaani nao wapate fursa ya kupata chanjo hiyo ili kuwakinga na saratari na mlango wa kizazi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akizungumza kwenye uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi iliyofanyika kimkoa katika Shule ya Msingi Kisaki Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

“Tunapoenda kuwalinda watoto wa kike kwa kuwachanja chanjo hiyo maana yake tunawaepusha na madhara ugonjwa wa saratani ili wasije wakaambukiza wavulana”Ameeleza RC. Halima Dendego.

Amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni muhimu kwa wasichana na inatolewa bure kwa sababu Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo imegharamia chanjo hiyo, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ili kuwaepusha na madhara yanayoweza kutokea. 

Kwaupande wake, Mganga Mkuu mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick amesema kwa Tanzania chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) ilianza majaribio mwaka 2014 mkoani Kilimanjaro na kupata mafanikio makubwa kwa kuwakinga wasichana wasipate ugonjwa huo.

Dkt. Victorina Ludovick ameeleza mtu yeyote anaweza kuambukizwa saratani hiyo katika umri wowote ule hasa wakati wa tendo la ndoa na inaweza kusababisha magonjwa mengine ikiwemo saratani ya koo na magonjwa mengine ya via vya kizazi kwa wanamke na wanaume.

Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amewataka Maafisa Afya wanaotoa chanjo hiyo kuhakikisha wanafanikisha zoezi hilo kwa viwango ili mkoa wa Singida uwe wa kwanza katika utoaji wa chanjo hiyo kwa wasichana mwenye umri wa miaka Tisa hadi 14.  

Amesema saratani hiyo inaua na ni ugonjwa hatari hivyo ni muhimu kwa watoto wote wenye umri wa kupata chanjo wapewe kutokana na umuhimu wake katika kulinda afya zao.

Nao, Mashuhuda waliopewa chanjo hiyo wakizungumza kwenye uzinduzi wa utoaji wa chanjo ya satarani la mlango wa kizazi katika kijiji cha Kisaki Manispaa ya Singida Lukuresia Andrea na Salisabila Athumani wote wakazi wa mkoa wa Singida wamesema tangu wapatiwe chanjo hiyo hawajapata madhara yoyote hivyo wameomba wazazi na walezi wasiwazuie watoto wao wa kike kwenda kupata chanjo hiyo kwa sababu inafaida kubwa katika maisha yao.


Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akizungumza kwenye uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.

Zoezi la kuimarisha chanjo ya HPV litakamilika tarehe 26 Aprili, 2024 hata hivyo hudumaa hiyo itaendelea kutolewa kwa utaratibu wa zamani yaani shuleni, vituo vya kutolea huduma za afya na kwenye huduma za mkoba za Masuala ya Afya ya Uzazi na Mtoto.

Chanjo ya HPV, kama ilivyo kwa chanjo nyingine zinazotolewa kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo, haiuzwi kwa mteja yeyote, hivyo inatolewa bure kwa walengwa katika vituo vyetu vya kutolea huduma.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego (mwenye koti rangi nyekundu), akiwa na wanawake waliopata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Singida waliokaa na watoto wao, Pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Baadhi ya Wanawake waliopata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Singida wakiwa na watoto wao.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Victorina Ludovick, akisoma taarifa ya utoaji wa chanjo katika Mkoa huo.

Wanafunzi kutoka Shule mbalimbali waliohudhuria kushuhudia na kupata huduma wakati wa zoezi la uzinduzi utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi katika kijiji cha Kisaki Manispaa ya Singida.



No comments:

Post a Comment