Monday, December 17, 2018

UFAULU DARASA LA SABA 2018, WAONGEZEKA NA WANAFUNZI WOTE WALIOFAULU WAMECHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2019


MKOA wa Singida umefanikiwa kujikwamua kutoka nafasi ya mwisho mwaka jana hadi nafasi ya 14 mwaka huu kwenye Mtihani wa kuhitimu Darasa la Saba Kitaifa. 

Afisa Elimu wa mkoa wa Singida, Nelasi Mulungu alikiambia Kikao cha Uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2019 mjini hapa kuwa mkoa umeweza kunyakua nafasi hiyo baada ya kufaulisha jumla ya wanafunzi 20,617 ikiwa ni sawa asilimia 75.21. 

Alisema kuwa kiwango hicho cha ufaulu ni ongezeko la asilimia 13.21 ikilinganishwa na asilimia 61.97 mwaka jana.

Mwl. Mulungu alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 27,412, kati yao wavulana 12,668 na wasichana 14,741 walifanya Mtihani, hivyo watahiniwa zaidi ya 6,700 hawakuweza kufaulu Mtihani huo. 

Kwa mujibu wa Afisa Elimu huyo, Halmashauri iliyofanya vizuri zaidi kati ya saba zilizopo mkoa wa Singida ni Itigi kwa asilimia 84.56 huku ikishika nafasi ya 50 Kitaifa, Singida Manispaa inafuatia kwa asilimia 81.95, Halmashauri ya wilaya ya Singida 81.02, Manyoni 77.34,  Ikungi (74.77),  Iramba (74.73) na Mkalama ufaulu wa asilimia 57.87 na hivyo kushika nafasi ya 7 kati ya halmashauri 7 kimkoa. 

Mwl Mulungu alisema licha ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kushika nafasi ya mwisho kimkoa lakini ufaulu wake umeongezeka hadi kufikia asilimia 57 ikilinganishwa na mwaka jana ilipokuwa na asilimia 37.08 jambo ambalo linapaswa kujivunia.

Alisema kuwa Wanafunzi waliofanya Mtihani mwaka huu ni asilimia 75.24 tu ya idadi yote ya wanafunzi 36,427 waliandikishwa Darasa la Kwanza 2012, hali inayoonesha wazi kuwa zaidi ya wanafunzi 9,000 waliacha shule njiani kwa sababu mbali mbali, ikiwemo kufariki, mimba, utoro na uhamisho. 

Alitaja baadhi ya mikakati ya kuendelea kuinua kiwango cha ufaulu kimkoa kuwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha kuwa walimu wanafanya maandalizi ya ufundishaji na kufundisha kikamilifu. Pia mikakati mingine ni kuandaa mitihani miwili ya utamilifu kwa wanafunzi wa darasa la Saba na la Nne. Aidha, kila mwezi kutakuwa na uwasilishaji wa upimaji kwa madarasa hayo kutoka katika kila Halmashauri kwa kila shule.

Kwaupande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Mhandisi Paskasi Muragili, aliutaka uongozi wa mkoa na wadau wa elimu kwa ujumla kuunganisha nguvu pamoja ili kuisaidia Halmashauri ya wilaya ya Mkalama ili iweze kufanya vyema zaidi hapo mwakani.

Mhe. Mhandisi Muragili alisema kuwa, halmashauri ya Wilaya ya Mkalama inahitaji nguvu ya Mkoa ili kumaliza changamoto mbalimbali zinazosababisha wasifanye vizuri zaidi katika matokea ya mitihani ya shule za msingi ikiwemo mazingira yaliyoizunguka Halmashauri ya Wilaya hiyo iliyogawanywa kutoka wilaya mama ya Iramba.

Alizitaja miongoni mwa changamoto hizo ni uhaba wa Walimu, mwamko duni kwa baadhi ya familia, jamii ya wafugaji, umasikini na hata jamii ya Wahadzabe kuwemo katika wilaya hiyo, hivyo kuhitajika nguvu ya ziada ili kuikwamua.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Singida alisema ingawa hiyo siyo wilaya yake kiutawala, lakini iwapo itasaidiwa kimkakati basi huenda ikasaidia kuchangia mkoa mzima wa Singida kufanya vyema zaidi na hata kuwa miongoni mwa mikoa mitano bora katika ufaulu wa matokeo ya darasa la saba hapo mwakani.

MATUKIO KATIKA PICHA
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu Mwl Nelasi Mulungu akizungumza wakati wa kikao.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Bw. Buhacha Baltazari Kichinda ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi - Utawala na Rasilimaliwatu mkoa wa Singida akifungua kikao.

 Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida Mwl. Ayubu Mchana akitoa miongozo mbalimbali wakati wa kikao.


Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Mhandisi Paskasi D. Muragili akizungumza wakati wa kikao.


 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Miraji J. Mtaturu akizungumza wakati wa kikao.


 Mkurugenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Singida Bw. Rashidi M. Mandoa akizungumza wakati wa kikao.

  Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya Itigi Mhe. Ally J. Minja akizungumza wakati wa kikao.


Mstahiki Meya, Halmashauri ya Manispaa ya Singida Mhe. Gwae C. Mbua akizungumza wakati wa kikao.


Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya Ikungi Mhe. Ally J. Mwanga akizungumza wakati wa kikao.



 Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu Mwl. Nelasi Mulungu akiwasilisha taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa KIDATO CHA KWANZA mwaka 2019 mkoa wa wa Singida, wakati wa kikao.

Afisa Elimu Taaluma Mkoa Singida Mwl. Ayubu Mchana akinakili jambo wakati wa kikao.


Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu Mwl. Nelasi Mulungu akizungumza na waandishi wa Habari mkoa wa Singida mara baada ya kumalizika kikao cha kutangaza matokeo na kupokea taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2019 mkoani Singida.

Imetolewa na;
Kitengo cha Habri na Mawasiliano,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
SINGIDA

No comments:

Post a Comment