Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kampasi ya Singida, kimekamilisha ujenzi wa majengo matatu katika awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho kwa gharama ya Shilingi 1,381,910,020.
Majengo yaliyojengwa katika awamu hii ni pamoja na majengo mawili ya madarasa na jengo moja la choo cha nje. Jengo la kwanza lina madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 150 kila moja, ofisi sita, ukumbi mdogo mmoja na vyoo vya nje viwili. Jengo la pili lina madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 90 kila moja, ofisi sita na ukumbi mdogo mmoja. Jengo la tatu ni choo cha nje chenye matundu tisa.
Awamu ya pili ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa majengo 30 katika kampasi hiyo. Majengo hayo ni pamoja na jengo la maabara ya kuchapia (typing laboratory), majengo ya madarasa, jengo la utawala, jengo la maktaba, ukumbi wa shughuli mbalimbali, ukumbi wa kisasa wa mikutano, zahanati, nyumba za wafanyakazi, maabara ya kompyuta, hosteli, jengo la mlezi wa wanachuo pamoja na jengo la mapumziko (rest house). Gharama ya jumla ya mradi mzima hadi kukamilika ni Shilingi 15,016,823,777.
Katika taarifa ya maendeleo ya mradi huo iliyowasilishwa mbele ya timu ya ukaguzi wa miradi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Chuo kilieleza kuwa hatua inayofuata ni kuanza awamu nyingine ya ujenzi wa mabweni ya wanachuo. Hii inalenga kupunguza changamoto ya wanafunzi wengi kulazimika kuishi katika hosteli za watu binafsi kutokana na ukosefu wa mabweni ya kutosha.
Kadhalika uongozi wa Chuo pia umetoa wito kwa wawekezaji kujitokeza na kushiriki katika ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanachuo, kwa kuwa uhitaji wa huduma hiyo bado ni mkubwa.
Timu ya ukaguzi wa miradi kutoka Mkoa wa Singida iliongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Daktari Fatuma Mganga, huku timu ya ufuatiliaji kutoka Manispaa ya Singida ikiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bi. Joanfaith Kataraia.
No comments:
Post a Comment