Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama
wametakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kufuata taratibu za kazi ambazo
ndizo zitakazoleta mafanikio ambapo wamekumbushwa kwamba lengo la uwepo wao ni kuwaletea maendeleo
wananchi husika na sio vinginevyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Binilith Mahenge alipokutana na kufanya kikako cha pamoja na viongozi
mbalimbali wakiwemo wakuu wa Idara katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo alielekeza Watumishi
kufuata taratibu za utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na
kufanya kazi kwa kushirikiana.
RC Mahenge amesema pamoja na kwamba Wilaya ya Mkalama
inafanya kazi nzuri ya makusanyo ya mapato lakini bado kuna changamoto zinazosabishwa na usimamizi usioridhisha
hivyo kuwataka wakuu wa Idara kuhakikisha wanashirikiana ili kuondoa changamoto
za miundombinu ya Barabara, Elimu, Afya, Amani na usalama pamoja na kuhakikisha
maendeleo yanatamalaki Wilayani hapo.
Hata hivyo Dkt. Mahenge amewapongeza Viongozi wa Wilaya hiyo
kwa hatua ambazo wamezifikia katika kutatua changamoto ndogondogo za migogoro
ya mipaka katika baadhi ya maeneo katika Kata ya Mwangezi wanapoishi jamii ya wahazabe na kuwataka kufikia
mufaka kwa njia ya majadiliano ili kuhakikisha Amani inaendelea kutawala maeneo
hayo.
Awali akitoa taarifa ya moja ya eneo lenye changamoto ya
migogoro wa Mipaka Diwani wa Kata ya Mwangeza ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bosco Charles Samweli amesema Kata yake
imekuwa na changamoto ya migogoro ya mpaka baina ya watu jamii ya Wahazabe na
wengine wa Mkoa wa Arusha na Manyara jambo ambalo halina Afya nzuri kwa Amani
ya Kata hiyo.
Ameiomba Serikali kuendeleza juhudi zake za kutatua
changamoto hiyo ambapo shughuli za maendeleo kwa jamii hizo zimesimama
wakisubiri majadiliano yanayoendelea baina ya viongozi wa mikoa hiyo.
Aidha Diwani ameomba msaada wa haraka kwa wataalamu wa
wanyamapori ili kusaidia kuondoa changamoto ya uvamizi unaofanywa na wanyama
pori wakiwemo Tembo na Simba katika mashamba ya wanakijiji ambapo mashamba yao
yamekuwa yakiharibiwa na Serikali ilishindwa kulipa fidia kwa wakulima hao.
Akitolea majibu changamoto hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama
Sophia Kizigo amesema Serikali hailipi fidia kwa wakulima bali inalipa kiasi kidogo cha kifuta machozi au pole kwa
walikutwa na dhahama ya kuvamiwa na wanyama na kuharibiwa kwa mazao yao.
DC Kizigo amesema kwamba tayari mawasiliano yameshaanza
kufanyika ili kusaidia kuwapangia kazi hiyo
wataalamu wa wanyamapori ili kukabiliana na changamoto hiyo huku
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akikiri kutengwa
eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya zoezi hilo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa Idara na vitengo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya pamoja na timu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo lengo la kikao hicho ilikuwa ni kuangalia changamoto zinazokabili Kata ya Mwangeza Wilayani hapo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment