Saturday, January 10, 2026

CHANGAMOTO ZA WAFUGAJI NA WAVUVI SINGIDA ZAANZA KUPATIWA UFUMBUZI

 


Posted on: January 10th, 2026

Wananchi wa Wilaya za Iramba na 
Mkalama mkoani Singida wameeleza matumaini mapya baada ya ziara ya kikazi ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Bashiru Kakurwa (Mb), iliyofanyika leo tarehe 10 Januari 2025, wakisema imefungua fursa ya kusikilizwa na kushughulikiwa changamoto zinazowakabili katika sekta ya mifugo na uvuvi.

Katika Wilaya ya Iramba, wananchi na viongozi wa wilaya walieleza kuwa uchumi wa eneo hilo unategemea kwa kiasi kikubwa ufugaji na uvuvi katika Ziwa Kitangiri. Mkuu wa Wilaya alibainisha kuwa wilaya ina idadi kubwa ya mifugo lakini bado inakabiliwa na upungufu wa miundombinu ya kisasa kama machinjio, minada na majosho, pamoja na uhaba wa watumishi wa mifugo na uvuvi. Alisema hali hiyo imekuwa ikiwalazimu wananchi kutumia gharama kubwa kupata huduma na wakati mwingine kushindwa kufikia masoko yenye tija.

Afisa Uvuvi wa wilaya alieleza kuwa shughuli za uvuvi zinaendelea kufanyika licha ya changamoto za vifaa na rasilimali, akibainisha kuwa wilaya ina wavuvi hai 204, mitumbwi 34 iliyosajiliwa na boti moja pekee. Alisema bado kuna hitaji kubwa la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi, kutoa elimu ya uvuvi endelevu kwa wananchi na kuboresha miundombinu ya uvuvi ili kuongeza tija na kipato cha wavuvi.

Katika Wilaya ya Mkalama, Mkuu wa Wilaya Mhe.Moses Machali alisema migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa changamoto ya muda mrefu, hasa katika maeneo ya mipakani, akisisitiza kuwa kuwekwa kwa mipaka rasmi kati ya Wilaya ya Mkalama na Meatu ni hatua muhimu ya kudhibiti migogoro hiyo. Aliongeza kuwa kuna haja ya kulifufua shamba la mifugo la Serikali lililotelekezwa na kuvamiwa, ili kulinda mali ya umma na kutoa mfano wa ufugaji wa kisasa kwa wananchi.

Wananchi wa Kijiji cha Nyahaa walieleza kero zao kuhusu uvamizi wa mifugo, wizi na migogoro iliyosababisha majeruhi na hasara za mali, wakisisitiza umuhimu wa Serikali kuchukua hatua hatua za haraka kurejesha amani na kuimarisha ulinzi wa mifugo.

Kwa ujumla, wananchi walisema ziara hiyo imeongeza uwazi na matumaini mapya, huku viongozi wa wilaya na wataalamu wa sekta wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ili kuboresha huduma za mifugo na uvuvi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Singida.





No comments:

Post a Comment