Saturday, March 16, 2019

JINA LA MWANAMKE ALIYEKUWA SHUJAA MKOA WA SINGIDA LETI HEMA (MAREHEMU), KUORODHESHWA NA MAJINA YA WATU MAARUFU NCHINI.


SERIKALI imeahidi itahakikisha jina la mwanamke aliyekuwa shujaa mkoa wa Singida Leti Hema (marehemu), linaorodheshwa na majina ya watu maarufu nchini akiwemo chief Mkwawa wa Iringa, kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Ahadi hiyo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokuwa mkoani Singida baada ya kutembelea pango alilokuwa akijificha Leti kukwepa askari wa kikoloni kutoka Ujerumani katika miaka ya 1850.

Inaelezwa Leti alikuwa ni mwanamke shujaa aliyepambana na askari wa kikoloni enzi  Tanganyika ikiwa chini ya wakoloni wa Kijerumani.

Leti ambaye inadaiwa alikuwa na utamaduni wa kutembea akiwa amebeba mkuki wakati wote, ndiye aliyeongoza mgomo wa Wanyaturu sehemu ya kaskazini, dhidi ya ukoloni wa Kijerumani.

Imeelezwa zaidi kuwa mwanamke huyo alikataa utamaduni wa aina yoyote ule kutoka nje ya Tanganyika, kwa wakati huo wa miaka ya 1850 na kuendelea.

Kwa mujibu wa kitabu cha Wanyaturu wa Singida, mila na desturi zao kilichoandikwa na Patrick Mdachi, ni kwamba Leti kwa nguvu na msimamo wake alijulikana Unyaturuni kote.

Kwa hiyo alijizolea sifa zilizopelekea achaguliwe  kuwa kiongozi wa mgomo. Kitendo hicho kilichopelekea asakwe na jeshi la wakoloni Wajerumani.

Kwa uwezo, ujasiri na akili alizaokuwa nazo, aliweza kuwafukuza wanajeshi hao kwa kutumia nyuki. Nyuki hawa kwa nguvu zake Leti aliweza kuwakusanya pamoja.

Kwa mujibu wa kitabu cha Mdachi, Wanajeshi hao wazungu walipomkaribia mwanamke huyo jasiri kwa lengo la kumuawa, alifungulia nyuki hao ambao waliwauma wazungu pekee kutokana na weupe wao. Wanajeshi hao waliweza kukimbia kuokoa maisha yao.

Imeelezwa jeshi hilo liliporudi tena mara ya pili kwa ajili ya kumsaka Leti ili wamuue, hatimaye lilifanikiwa kumua mwanamke huyo jasiri.

Hali hiyo ndiyo iliyompelekea mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezi nchini Dk. Harrison Mwakyembe kusema, kutokana na ushupavu wa hayati Leti, kuna umuhimu mkubwa jina lake kuwemo kwenye orodha ya watu maarufu kama njia ya kuenzi uzalenzo wake.

“Hili jina la Leti, ni lazima lipewe heshima stahiki. Kwenye bunge linalotayajiwa kuanza vikao vyake karibuni, nitalisimamia kuhakikisha linatambulika ili mwanafunzi shuleni anaposikia jina hili la Leti likitajwa awe analifahamu na awe na uwezo wa kulielezea kwa undani” Mhe. Dk. Mwakyembe amesisitiza.

Aidha, Waziri Mwakyembe amemwagiza mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Singida, kuhakikisha jabali la mawe la Ipembe lililopo katika Manispaa ya Singida, kusitishwa shughuli za kibinadamu zinazofanyika hapo zikiwemo za kilimo, ujenzi wa nyumba, ili kuhifadhi mandhari nzuri ya jabali hilo ikiwa kama sehemu ya kivutio cha utalii na utamaduni.

Pia, ameagiza eneo lote la jabali hilo, lipandwe miti na kwa ujumla lirejeshwe kwenye uhalisia wake.

“Majabali  kama haya yenye umuhimu wa aina yake, ni lazima yatunzwe na kulindwa kikamilifu. Jabali hili ni kivutio tosha. Tusiruhusu litumike kwa matumizi ya aina yoyote ya kibinadamu ikiwemo kujenga hoteli kama nilivyosikia”, Dk. Mwakyembe.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Singida, Mheshimiwa Mhandisi Pascas Muragili amemuahidi mheshimiwa Waziri kusimamia jambo hili kikamilifu na akatoa onyo, na marufuku kwa mtu yeyote kufanyika shughuli zo zote za kibinadamu katika eneo lote la jabali la Ipembe.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA;
ZIARA YA WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO 
MHE. DR. HARRISON MWAKYEMBE, MKOANI SINGIDA.


 Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe akisalimiana na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Singida alipokuwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika halmashauri ya wilaya ya Singida mkoani Singida.

 Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe akizungumza jambo na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Singida wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.

 Mkuu wa wilaya ya Singida Mheshimiwa Mhandisi Pascas Muragili akimuelezea jambo Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe alipotembea jengo la kihistoria katika halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.

 Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.

 ENEO LA NG'ONGO IPEMBE


  Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe akiwa ameketi juu ya jiwe lililopo katika bonde la ufa alipokuwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.



Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe (watatu kutoka kushoto) akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria KILIMATINDE, katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.





 (Boma la Mjerumani)

 Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika halmashauri ya Mkalama mkoani Singida.

Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Singida

No comments:

Post a Comment