Tuesday, November 18, 2025

RC DENDEGO ASISITIZA UBUNIFU KATIKA UANDAAJI WA TAKWIMU

 

.                           

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameongoza kikao cha Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika 2025 kwa ngazi ya kanda kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Novemba 18,2025, Kikao  kilichowakutanisha wadau kutoka mikoa ya Manyara, Morogoro, Dodoma na Singida kwa lengo la kujadili umuhimu wa takwimu katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Dendego alisema matumizi ya takwimu sahihi ni nyenzo muhimu ya kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, hasa katika kipindi ambacho dunia inapitia mageuzi ya teknolojia.


Amesisitiza kuwa ni muhimu wadau wote wakiwemo serikali, sekta binafsi na taasisi za kiraia kuongeza ubunifu katika ukusanyaji na matumizi ya takwimu ili kuhakikisha maamuzi yanayofanyika yanakuwa na tija kwa jamii. Aidha, alitoa pongezi kwa waandaaji wa maadhimisho hayo kwa kulipa uzito kundi la wanahabari, akieleza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kufikisha taarifa sahihi kwa umma na mara nyingi hutumia takwimu kama msingi wa habari zao.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Bw.Naing'oya Kipuyo, alisema takwimu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa kwa kuwa zinawezesha serikali na wadau kupanga miradi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi. Alieleza kuwa takwimu sahihi huimarisha uwajibikaji na utawala bora, kwani viongozi wanawaletea wananchi taarifa za uhakika kuhusu rasilimali na huduma za kijamii. Aidha, alibainisha kuwa takwimu hutumiwa na wawekezaji kutambua fursa za kiuchumi na kufanya maamuzi sahihi, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi na kujenga mazingira bora ya biashara.

Bw. Kipuyo aliongeza kuwa takwimu rasmi husaidia kudhibiti upotoshaji wa taarifa na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu hali ya sekta mbalimbali kama elimu, afya na ajira. Alifafanua kuwa takwimu ndizo msingi wa kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hivyo kusaidia taifa kutambua maeneo yanayohitaji maboresho. Aidha, alisema mchakato wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu unachochea matumizi ya teknolojia na ubunifu katika taasisi za umma na binafsi, na hivyo kuwezesha maamuzi yenye tija yanayochangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Miongoni mwa watoa mada katika maadhimisho hayo alikuwa Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Nipashe mkoa wa Singida, Thobias Mwanakatwe. Katika mada yake, Mwanakatwe alieleza kuwa matumizi sahihi ya takwimu rasmi na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kujenga jamii inayojali haki, amani na maendeleo. Alisema takwimu zinapowasilishwa kwa umma kwa usahihi na uwazi husaidia wananchi kuelewa hali halisi ya sekta mbalimbali kama elimu, afya, uchumi na huduma za kijamii.

Aidha, Mwanakatwe alibainisha kuwa takwimu rasmi zinapochambuliwa na kuripotiwa vyema na vyombo vya habari husaidia kuzuia upotoshaji, kuimarisha uwajibikaji wa viongozi na kufanya maamuzi yenye tija kwa jamii. Alisisitiza kuwa vyombo vya habari vinapozingatia ukweli wa takwimu vinakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kijamii badala ya kuwa chanzo cha migogoro au upotoshaji. Pia aliongeza kuwa uandishi wa habari unaotumia takwimu rasmi huibua maeneo yanayohitaji maboresho na kuimarisha misingi ya utawala bora.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kuongeza ubunifu katika matumizi ya takwimu na taarifa ili kujenga jamii jumuishi inayojali haki, amani na maendeleo kwa Waafrika.” Kaulimbiu hii inalenga kusisitiza umuhimu wa matumizi bunifu ya takwimu katika kuimarisha utawala bora na ustawi wa jamii.








No comments:

Post a Comment