Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Daktari Fatuma Mganga, amewaagiza Wakuu wa Sehemu, Idara na Vitengo kuhakikisha wanazalisha matokeo mazuri na chanya kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali, sambamba na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika miradi inayotekelezwa.
Daktari Mganga alitoa maagizo hayo leo wakati wa kikao cha Kamati ya Bajeti cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika ofisi za Sekretarieti ya Mkoa wa Singida.
Amesema ni muhimu kwa viongozi kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija kwa wananchi, sambamba na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika kikao hicho, wajumbe walijadili masuala mbalimbali yakiwemo taarifa za utekelezaji wa bajeti, mpango wa matumizi ya fedha, pamoja na changamoto za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo.
Aidha, Katibu Tawala ametoa pongezi kwa vitengo vya Sheria, Ugavi na Ununuzi, Miundombinu na Uhasibu kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha na kufanikisha miradi kadhaa kukamilika kwa ubora wa hali ya juu.
Akihimiza uwajibikaji, Dkt. Mganga aliwataka viongozi wote kuwasimamia watumishi waliopo chini yao katika kujaza ipasavyo mfumo wa upimaji wa utendaji kazi wa watumishi (PEPMIS) kulingana na majukumu wanayoyatekeleza. Pia aliagiza kila kiongozi kutambua viashiria vya utendaji vinavyopima mafanikio ya idara yake ili kuhakikisha utekelezaji bora wa majukumu yao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo, pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya za mkoa wa Singida. Kikao hicho kiliendeshwa na Katibu Tawala wa Mkoa, huku Katibu wa kikao hicho akiwa Bw. Nesphory Bwana, Katibu Tawala Msaidizi – Sehemu ya Mipango na Uratibu.








No comments:
Post a Comment