Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka viongozi wa sekta ya afya kuhakikisha wanapunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga, akisisitiza umuhimu wa kutumia ipasavyo rasilimali zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ametoa maagizo hayo katika kikao cha kujadili mwenendo wa vifo vya kina mama na watoto wachanga kwa robo ya Julai hadi Septemba 2025 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida, ambapo amewataka wakurugenzi wa halmashauri na waganga wakuu wa wilaya kuongeza uwajibikaji na ubunifu katika kuboresha huduma za afya.
Dkt. Mganga amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kupitia ujenzi wa miundombinu, usambazaji wa vifaa tiba, na kuongeza bajeti ya dawa, hivyo viongozi wa afya wanapaswa kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa tija ili kuokoa maisha ya wananchi. “Serikali imeleta miundombinu na vifaa kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunavitumia kupunguza vifo vya kina mama na watoto,” amesema.
Akiendelea kutoa maagizo, Dkt. Fatuma amewataka waganga wakuu na wakurugenzi kutoa elimu kwa wanawake na wanaume hata kabla ya kupata ujauzito, ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu afya ya uzazi na kuzuia vifo vinavyotokana na kukosa elimu. “Tusichague hadhira ya kuielimisha, watu sahihi si wale wanaokuja hospitalini wakiwa wajawazito tayari. Tuelimishe jamii nzima wajue namna ya kujiandaa na kutunza ujauzito wenye afya bora,” amesema.
Pia amezitaka kamati zote zinazohusiana na ufuatiliaji wa vifo vya kina mama na watoto wachanga kuimarishwa, huku akiwasihi wananchi kutumia vituo vya afya vilivyo karibu wakati wa dharura badala ya kusafiri umbali mrefu, ili kuokoa maisha ambayo yangepotea kwa kuchelewa kupata huduma.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick, amesema kuwa wakina mama hupoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokwa na damu nyingi na matatizo ya upumuaji kwa watoto wachanga. Amesema uongozi wa afya umeongeza jitihada katika kuhakikisha dawa zinapatikana, huduma za rufaa zinaboreshwa, na magari ya wagonjwa yanakuwa tayari muda wote kwa ushirikiano na madereva jamii.
Viongozi wa hospitali na waganga wakuu wa halmashauri zote za Singida wameahidi kuendelea kushirikiana katika kutoa elimu, kuongeza uwajibikaji na kutumia kwa ufanisi rasilimali zilizotolewa na Serikali ili kuhakikisha vifo vya kina mama na watoto wachanga vinapungua kwa kiwango kikubwa.





No comments:
Post a Comment