Wednesday, August 30, 2017

KANISA LA RC LAPONGEZWA KUWAFUNDISHA VIJANA KULIPA KODI.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe na Askofu Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Edward Mapunda wakipongezana kwa kazi nzuri ya kuwaelimisha vijana katika kongamano la vijana wa kanisa katoliki jimbo la Singida.
Baadhi ya vijana Kanisa Katoliki Jimbo la Singida waliohudhuria kongamano la wiki moja, lililofanyika kwenye jukwaa la Askofu Mabula mjini Singida.

Mbuge Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, amelipongeza kanisa la Romani Katoliki (RC) jimbo la Singida kwa uamuzi wake wa kuwaelimisha vijana 490 umuhimu wa kulipa kodi.

Mattembe ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye kongamano la vijana waumini wa kanisa hilo lililofanyika kwenye jukwaa la askofu Mabula kwenye viwanja vya kanisa katoliki mjini hapa.

Amesema vijana wakiwezeshwa kutambua mapema umuhimu wa kulipa kodi na manufaa yake, nchi itakuwa ya walipa kodi ambao watalipa kwa hiyari yao bila kushurutishwa. 

“Suala la kulipa kodi ni muhimu mno kwa maendeleo ya nchi yo yote hapa duniani. Rais wetu Dkt Magufuli ameleta mageuzi makubwa mno yanayohusu kulipa kodi. Anajua umuhimu wa kulipa kodi kwa sababu bila kodi hakuna maendeleo. Baba Askofu, kitendo chenu cha kutoa elimu ya kodi kwa vijana hawa mtakuwa mmemuunga mkono rais Magufuli na hongereni sana”, amesema Mattembe.

Mbunge huyo amewataka vijana hao ambao wametoka wilaya zote za mkoa wa Singida,wakawe mabalozi wazuri katika kueneza elimu ya kulipa kodi kwa wenzao ambao hawakubahatika kuhudhuria kongamano hilo.

 “Vijana wenzangu haya maendeleo makubwa mnayoyaona ya barabara nzuri, vituo vya afya na visima vya maji na maengine mengi, yote yanagharamiwa na fedha za kodi na si vinginevyo. Serikali ya awamu ya tano inamtaka kila mtanzania mwenye sifa ya kulipa kodi alipe, tena kwa wakati bila ya kushurutishwa”, amesisitiza.

Aidha amaewataka vijana wote mkoani hapa wenye sifa ya kufanya kazi, wajiunge kwenye vikundi vya ujasiariamali pamoja na vile vya kilimo cha biashara, ili waweze kujiletea maendeleo na kujikomboa kiuchumi.

“Faida za kujinga kwenye vikundi vilivyosajiliwa ni nyingi ikiwemo ya kupata mikopo kwa masharti nafuu kutoka taasisi za kifedha. Tunayo maeneo ya kutosha kwa ajili ya ufugaji nyuki. Mazao ya nyuki yana soko kubwa ndani na nje ya nchi. Anzisheni vikundi vya ufugaji nyuki mtaharakisha kujikomboa kiuchumi. Nina uhakika serikali ya mkoa na ofisi yangu tutawasaidia ili muweze kufikia malengo yenu”, amesema.

Mattembe ameahidi kuchangia mizinga ya kisasa ya kutosha kwa vijana watakaojiunga katika vikundi huku akiungwa mkono na Katibu wa Jumuiya ya Wanawake (CCM) Manispaa ya Singida Magreth Malecela ambaye ameahidi kuchangia mizinga mitano ya kisasa.

Awali Baba askofu wa jimbo la Singida Edward Mapunda amesema vijana hao pia wamepewa elimu juu ya ujasiriamali, kilimo cha biashara na maadili mema.

Aidha, amesema kongamano hilo ambalo linafanyika kila mwaka mara moja, linatarajia kupanua wigo kwa kupata wawezeshaji wa fani mbalimbai kutoka nje ya mkoa.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe akitoa nasaha zake kwenye kongamano la vijana wa kanisa katoliki jimbo la Singida.

Baba Askofu Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Edward Mapunda akizungumza kwenye kongamano la juma la vijana kanisa katoliki. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe.

No comments:

Post a Comment