Timu ya Ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Fatuma Mganga, imefanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya Mkoa wa Singida iliyopo katika Manispaa ya Singida.
Mradi huu unatekelezwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi. Ujenzi huo unajumuisha jengo kuu la ofisi, ujenzi wa uzio (fensi), nyumba ya mlinzi, jumba la umeme (power house), mitaro ya maji pamoja na sehemu za maegesho (parking).
Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi bilioni 2.402.417.177 na hadi sasa uko katika hatua ya asilimia 30 ya utekelezaji. Kazi zilizofanyika mpaka sasa ni pamoja na ufungaji wa mifumo ya umeme katika jengo la ofisi, ufungaji wa mifumo ya kiyoyozi, mifumo ya maji taka, usukaji wa nondo pamoja na ujenzi wa kuta za nyumba ya mlinzi.
Baada ya ukaguzi huo, timu ilitoa maelekezo na mapendekezo kwa wakandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa. Miongoni mwa maelekezo hayo ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi, kutumia vyanzo mbadala vya maji, kuhakikisha mifumo ya TEHAMA ya serikali inawekwa kwa viwango vya juu kwa kuzingatia matumizi ya jengo hilo.
Aidha, imeelekezwa kuwa jengo hilo liwe rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu katika maeneo yote, gharama za fedha zionekane katika kazi inayoendelea, na kuwe na picha za mfano zinazoonesha sura ya mwisho ya jengo baada ya kukamilika. Vilevile, imeagizwa kuwa kazi zote zifanyike kwa ushirikiano na taasisi za usalama zikiwemo zimamoto ili kuhakikisha mifumo yote ya kiusalama inakidhi viwango vya kitaalam.
Timu hiyo pia imesisitiza umuhimu wa kupima ubora wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi ili kuhakikisha vinakidhi viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za ujenzi wa serikali.
No comments:
Post a Comment