Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego ametoa wito kwa viongozi wote Mkoani Singida kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili badala ya kuongeza matatizo mengine.
Ameyasema hayo siku ya jana Septemba 17,2025 wakati akiwahutubia wananchi katika maadhimisho ya Maulid yaliyofanyika katika eneo la Sheikh Mkuu wa Mkoa ambapo Mhe. Dendego aliwataka viongozi wote kuanzia ngazi ya juu hadi chini – wakuu wa wilaya, maafisa tarafa, na watendaji wa mitaa – kuwahudumia wananchi kwa ushirikiano na moyo wa kuhudumia.
"Wanapokuja watu wetu wakiwa na changamoto na matatizo, tusiwaongezee changamoto zingine, tuhahakishe tunashirikiana kuzitatua changamoto zao," alisema Mhe. Dendego kwa msisitizo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwahimiza wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura ifikapo Oktoba 2025 akisisitiza kuwa kila mtu ana wajibu wa kikatiba kushiriki uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano ili kuchagua viongozi bora watakaowaongoza kwa maendeleo ya taifa.
“Nenda kamchague yule unayemwamini kuwa atakuvusha kwa miaka mitano ijayo. Atakayejali maendeleo, maji, afya, elimu na barabara. Nenda ukaweke kura yako ya ndiyo,” aliongeza Mhe. Dendego. Alisisitiza kuwa serikali imejiandaa vyema kuhakikisha kila mtu anapiga kura kwa amani na kurejea nyumbani salama, kwa kuwa huo ndio utamaduni wa kitaifa unaozingatia utulivu na sheria.
Katika hotuba yake, aliwaasa vijana kuhakikisha wanazingatia maadili, kuwa na heshima katika kauli na matendo, kujiepusha na lugha chafu, na kutoiga tabia zisizofaa. Aliwahimiza kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uharibifu vinavyoweza kupelekea madhara ikiwemo magonjwa ya zinaa kama VVU. “Vijana mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuishi kwa upendo na ukarimu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Sheikh Swed Twalibu Mkiza, aliyemuwakilisha Mufti Mkuu wa Tanzania, Aboubakar Zubeir, alihimiza amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi. Aliwasihi wananchi na wanasiasa kutumia lugha ya staha katika kampeni, wakiepuka maneno au matendo yanayoweza kuchochea taharuki katika jamii.
“Tusimame katika uzalendo, tusisimame katika utaifa. Uzalendo ni hali ya mtu kulinda na kuthamini nchi yake, ilhali utaifa unapobeba dhana ya kuidharau nchi nyingine huzua ukabila na kusababisha kupotea kwa amani,” alisema Sheikh huyo.
Aidha, aliwaasa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhakikisha wanachangia mijadala inayolinda amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa badala ya kuchochea migawanyiko.
Katika kuunga mkono wito huo, kijana Aboubakar Sadick ambaye alihudhuria sherehe hizo, aliwaasa vijana wenzake kuenzi na kuishi maadili mema yanayofundishwa na dini pamoja na mila za Kitanzania ili kulinda amani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo. Alisisitiza umuhimu wa vijana kushiriki uchaguzi mkuu kwa kuchagua viongozi bora wenye dira ya maendeleo.
“Kupiga kura ni haki yangu na ni daraja la kunikutanisha na kiongozi bora ambaye atanivusha kimaendeleo katika jamii yangu. Nitaitumia kura yangu kwa busara kuchagua kiongozi ninaemwamini ili baadaye nijivunie mchango wake katika jamii,” alisema Aboubakar kwa msisitizo.
Kwa undani zaidi wa taarifa hii tafadhali tazama video iliyoambatishwa hapa chini👇
No comments:
Post a Comment