Monday, December 17, 2018

AGIZO LA MHE. RAIS LA KUWATAMBUA NA KUWAPATIA VITAMBULISHO WAJASIRIAMALI WADOGO LAANZA KUTEKELEZWA MKOANI SINGIDA


Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. REHEMA NCHIMBI ametekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, la kutoa na kuwagawia vitambulisho vya kuwatambua wajasiriamali wadogo wenye mauzo ghafi yasiyofikia kiasi cha shilingi milioni 4 kwa mwaka.

Akikabidhi vitambulisho hivyo mkoani Singida, Dkt. Nchimbi amewataka wafanyabishara hao kutumia fursa hiyo vizuri kwa kufanya biashara kwa nidhamu na uadilifu mkubwa kama hatua ya kuboresha maisha yao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.


“Mkivipata vitambulisho hivi, lazima kukivaa wakati wote katika shughuli zenu za kibiashara. Hazuiwi mjasiriamali eti kwasababu amepatia mkoani Singida basi abaki Singida, anauhuru na anahaki ya kwenda kufanya biashara mahali popote hapa nchini ilimradi popote atakapokuwapo avae kitambulisho hiki”. Amesisitia Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi alisisitiza,  Mmachinga aliyepata kitambulisho afanye biashara yake   kifua mbele bila kubughudhiwa na mamlaka yeyote.

“Ndugu zangu Wamachinga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli anawapenda sana wananchi wake na  amesikia kilio chenu ambapo mlikuwa mkinyanyaswa na kubughudhiwa. Lakini kwa sasa mko huru ilimradi mna  vitambulisho vyenu ambavyo mtakuwa mmevivaa shingoni hakuna mtu atakayewabughudhi”.

“Viambulisho hivi haviuzwi bali vinachangiwa kwa kila Mmachinga shilingi elfu ishirini  na unaweza kuvitumia mahali popote nchini na  vinatolewa na ofisi za  wakuu  wa Wilaya, hivyo natoa wito kwa Machinga wote katika Halmashauri  za  mkoa wangu wa Singida ili kuwaondolea  bughudha zinazowakabili wanapokuwa wakiuza bidhaa zao Machinga hawa wasisumbuliwe wala kubughudhiwa”. Alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi amewalipia vitambilisho hivyo baadhi ya  Machinga wenye uhitaji maalum (walemavu) na  viongozi wa dini mbalimbali za mkoani hapa ambao wamekidhi vigezo vinavyotakiwa na Serikali vya mtu kuwa Machinga. Pia aliwaomba Machinga hao watakaokuza mitaji yao na kuwa wafanyabiashara inawapasa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwani kodi  ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Singida  Bw. Apili Mbaruku alisema kuhusu vigezo vya kupata kitambulisho cha Machinga  ni pamoja na Machinga kuwa na kipato chini ya milioni nne. 

“Leo hii Mhe. Mkuu wa Mkoa utawapa vitambulisho Machinga 53 ambao wamekidhi vigezo ambapo kwa maelekezo tuliyopewa kila Machinga anawajibika kujaza fomu na kutia saini taarifa zake zilizo sahihi na endapo atatoa taarifa ya uongo mhusika atachukuliwa hatua stahiki”. Awali, Meneja Mbaruku alitilia mkazo. 

Bw. Mbaruku aliongezea kuwa, vitambulisho hivi vitasaidia kuboresha biashara za wajasiriamali ili waweze kuwa walipa kodi wazuri nchini. 

Naye Machinga anayefanya biashra ya kuchonga vitanda mtaa wa kambi ya fisi mjini hapa, Abdul Kachimba alisema amefarijika sana kupata kitambulisho cha Machinga  ambacho atakitumia kufanya kazi ya biashara yake kwa ufanisi zaidi. 

“Namshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Magufuli ambaye ametupa fursa pekee sisi wajasiriamali kutusaidia vitambulisho hivi  ambavyo vitasaidia kutambulika nchi nzima,  hii ni chachu ya kutusaidia kwenda kwenye maendeleo ya biashara zetu ambapo hatimaye tunaweza  kuwa wafanyabiashara wakubwa ambao tutasaidia kuongeza pato la Taifa” alisema Kachimba. 

Wafanyabishara wengine wadogo wa mkoa wa Singida wakipokea vitambulisho hivyo vya ujasirimali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa awamu ya Tano la kutambua na kuthamini kazi zinazofanywa na wafanyabiashara wadogo wenye mauzo ghafi chini ya milioni 4, wameshukuru kupatiwa vitambulisho hivyo ambavyo wamesema vitawaondolewa usumbufu katika ufanyaji wa biashara zao hapa nchini. 

Zoezi hili limefanyika sanjari na utoaji mafunzo kwa wafanyabiashara 1000 wa Manispaa ya Singida kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania - MKURABITA ambayo yatawawezesha wafanyabiashara hao kutambulika rasmi na hivyo kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kupata mikopo.

MATUKIO KATIKA PICHA 

















PICHA YA PAMOJA

Imetolewa na;
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
SINGIDA

No comments:

Post a Comment