Tuesday, December 11, 2018

MANISPAA YA SINGIDA UMEWEKA MKAKATI WA KUANZISHA KITUO CHA PAMOJA CHA USAJILI NA UTOAJI WA LESENI KWA WAFANYABIASHARA.



Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania MKURABITA kwa ushirikiano na Manispaa ya Singida umeweka mkakati wa kuanzisha kituo cha pamoja kwa ajili ya usajili na utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara.


Mkuu wa wilaya ya SINGIDA Mhandisi PASKAS MURAGILI amesema kituo hicho ambacho kitakuwa na Taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA  kitaondoa vitendo vya rushwa katika utoaji wa leseni za biashara kwa sababu huduma hiyo itakuwa inatolewa katika eneo moja na kwa uwazi.

Mhe. Muragili ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya urasimishaji na uendeleshaji wa biashara kwa Wafanyabiashara mkoani Singida yaliyofanyika jana katika ukumbi wa shule ya sekondari Mwenge katika Manispaa ya Singida

“Kufanya biashara katika maeneo ambayo hutambuliki inakuwa haina faida kubwa sana, kwasasa tunaweza kwenda kuwatambua, kuwaweka pamoja na kupata huduma zote katika kituo kimoja”. Amesema Mhe. Muragili.

Amesisistiza kuwa, kwakuanzisha kituo hicho kitawasaidia wafanyabiashara katika kukuza mitaji yao kwanjia ya mikopo kutoka katika taasisi za kibenki mara baada ya  mfanyabiashara kutambulika katika mfumo rasmi, hivyo amewataka wafanya biashara waliohudhuria mafunzo hayo kuitumia vyema fursa hiyo adimu ili kuondokana na biashara mazoea.

“Ndugu wafanyabiashara, kwa hakika napenda kuwahimiza washiriki wote kutumia mafunzo haya kwa umuhimu mkubwa sana,  ni vyema mkajivunia na kuona kwamba mnayofahari kubwa kuweza kushiriki mafunzo haya muhimu na adimu”  Amesema Mhe. Muragili.

Aidha, Mheshimiwa Muragiri amesema hatapenda kusikia mchezo wa rushwa unafanyika kwenye ofisi zitakazoanzishwa na watumishi watakaobanika kufanya hivyo basi watakiona kilichomtoa nyoka pangoni.

Naye, Mheshimiwa Meya wa Manispaa ya Singida Alhaji Mbua Chima amewahakikishia wafanyabiashara hao kupatikana kwa ofisi hiyo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kuwa pamoja wakati wote jambo ambalo litawarahisishia shughuli zao za kiofisi.

Kwa upande wao Wafanyabiashara na Wajasiriamali katika Manispaa ya Singida wameunga mkono uanzishwaji wa ofisi hiyo.

Mafunzo yaliyotelewa ni pamoja na elimu juu ya urasimishaji na uendeshaji wa biashara, taratibu za kupata leseni za biashara na faida zake, umuhimu wa kutunza biashara pamoja na kutenganisha mali binafsi na mali za biashara, taratibu za kufungua akaunti bank pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji ya biasha, umuhimu wa biashara na kulipa kodi za serikali, mbinu za kupata bidhaa na mbinu bora za masoko, bima za bidhaa na faida zake, umuhimu wa bima za afya, uchumi wa viwanda na umuhimu wa mfanyabiashara kuweka akiba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

MATUKIO KATIKA PICHA

 Mkuu wa wilaya ya Singida Mhe. Mhandisi. Paskasi Muragili akizungumza na wafanyabiashara wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Urasimishaji na Uendeleshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Singida mkoani Singida.

Sehemu ya wawezeshaji pamoja na maafisa kutoka taasisi mbalimbali  za kibenki wakifurahia jambo.

 Mkuu wa wilaya ya Singida Mhe. Mhandisi. Paskasi Muragili akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mara baada ya kufungua mafunzo ya Urasimishaji na Uendeleshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Singida mkoani Singida.

 Kaimu Mkurugenzi wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania MKURABITA Bw. Japhet Werema akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo ya Urasimishaji na Uendeleshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Singida mkoani Singida.

 Mheshimiwa Meya wa Manispaa ya Singida Alhaji Mbua Chima akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo ya Urasimishaji na Uendeleshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Singida mkoani Singida.

 Mfanyabiashara wa mjini Singida Bi. Happy Francis akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo ya Urasimishaji na Uendeleshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Singida mkoani Singida.

 Mjasiriamali wa mjini Singida Bi. Sabina Mwanga akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo ya Urasimishaji na Uendeleshaji wa Biashara kwa Wafanyabiashara katika Manispaa ya Singida mkoani Singida.





Mada mbalimbali zikiwasilishwa na wawezeshaji husika

PICHA YA PAMOJA

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano 
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 
SINGIDA

No comments:

Post a Comment