Wednesday, September 24, 2025

MRADI WA UMWAGILIAJI IRAMBA,WAKULIMA SHIDA YA MAJI KUISHA

Mradi wa Umwagiliaji wa Masimba unaotekelezwa katika vijiji vya Urughu na Masimba, kata ya Ndago, wilayani Iramba mkoani Singida, unaendelea na  utekelezaji wake huku ukitarajiwa kuwanufaisha wakulima wengi zaidi.

Mradi huu unajumuisha kazi za barabara za mashambani zimekamilika kwa asilimia 90.58, ambapo usafishaji na uwekaji wa vifusi jumla ya kilomita 21.67 umekamilika, huku kilomita 5.6 kati ya 9.25 za barabara zikiwa tayari. Kazi za maumbo ya umwagiliaji zipo kwenye asilimia 18.32, zikiwemo ujenzi wa vipunguza kasi 14 kati ya 47 na kalvati moja kati ya 25, wakati maandalizi ya mashamba yamefikia asilimia 16.93, ambapo hekta 132 kati ya 750 zimeshasawazishwa huku Mradi huu unagharimu shilingi bilioni 10.4 

Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Meneja wa Mradi Mhandisi Emmanuel Challo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiamini Tume na kuipatia fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji ikiwemo huu wa Masimba.

Mradi huo wenye jumla ya ekari 1800 unatarajiwa kunufaisha wakulima 730 kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji.


Timu ya ukaguzi wa mkoa ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, imependekeza kuongeza idadi ya watendaji wa mradi ili kazi zifanyike kwa kasi zaidi usiku na mchana, na hivyo wananchi waanze kunufaika mapema na mradi huo muhimu.























No comments:

Post a Comment