Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, leo amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya elimu katika Wilaya ya Iramba, akiwa ameambatana na timu ya ufuatiliaji ya Mkoa.
Akiwa katika Shule ya Msingi Ushora Utemini, kijiji cha Songambele, Kata ya Ndago, Katibu Tawala alikagua mradi wa ujenzi wa madarasa matatu, matundu sita ya vyoo pamoja na vyumba viwili vya madarasa ya awali na matundu aita ya vyoo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 143 kupitia fedha za BOOST. Mradi huo upo katika hatua za awali za maandalizi ambapo mchanga, kokoto na tofali tayari vimekusanywa, huku michango ya wananchi ikiendelea.
Aidha, Katibu Tawala alitembelea mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa 2-in-1 katika shule hiyo, mradi wenye thamani ya shilingi milioni 95 zilizotolewa na Serikali Kuu na nguvu kazi ya wananchi. Hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 53 zimetumika na kiasi cha shilingi milioni 44 kimebaki.
Mapendekezo yaliyotolewa baada ya ukaguzi huo uliofanyika ni pamoja na kuwataka viongozi wa shule na kamati za ujenzi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu, ikiwemo ununuzi wa milango na samani imara ili majengo yadumu kwa muda mrefu.
Aidha Daktari Mganga, amewaagiza walimu kuongeza bidii katika ufundishaji wanafunzi ili kuinua ufaulu, sambamba na utunzaji bora wa mazingira ya shule. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora chenye lishe ili kuboresha afya na uwezo wa kujifunza.
Kwa niaba ya wananchi na uongozi wa shule, Mkuu wa Shule ya Msingi Ushora Utemini, Mwalimu Julius K. Massawa, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa huruma na uwekezaji mkubwa aliofanya katika sekta ya elimu unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia wilayani humo.
No comments:
Post a Comment