Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga ameagiza kuongezwa kwa idadi ya Wataalam wa lugha ya alama(Wakalimani) katika maeneo mbalimbali ya Umma ya kutolea huduma za kijamii ili kutengeneza mazingira rafiki kwa viziwi wanaposhiriki katika mikutano,vikao ili kuwawezesha kupata huduma zilizo bora sambamba na kushiriki katika kutoa maamuzi yanayaowagusa wanajamii kwa ujumla.
Hayo yamezungumzwa leo Septemba 24,2025 katika eneo la Chuo cha VETA Mkoani Singida katika Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi duniani iliyowakutanisha Viziwi kutoka mikoa yote Tanzania,wakalimani sambamba na Maafisa Elimu maalum chini ya Kaulimbiu isemayo
"Bila lugha ya alama hakuna haki za binadamu"
Daktari Mganga ametoa Agizo kwa kila halmashauri kuhakikisha kuna mtaalam wa lugha ya alama,kadhalika katika mahospitali , katika mikusanyiko mikubwa ikiwemo masokoni na mikutanoni ili kusaidia kutoa huduma inapohitajika sambamba na wao kutoa maoni ya yabayowagusa.
"Viziwi wanahitaji elimu na huuma nyingine za kijamii,hivyo ni sahihi kanzidata kufanyika vizuri ili kufahamu idadi yao vema ili kuwarahisishia kupata huduma muhimu wananchi wanazitakiwa kuzipata ikiwemo huduma za elimu kwa wote watoto na watu wazima kupitia elimu ya watu wazima,kadhalika huduma za kifedha katika benki,mikopo mbalimbali"
Kadhalika amewaagiza Maafisa ustawi wa jamii Nendeni mkahakikishe mnapata idadi kamili ya Viziwi ili kupata takwimu sahihi,lengo kuu ni kuhakikisha wote wanapata elimu kwani ndiyo msingi wa kila jambo na baadae kujiunga na elimu za Vyuo na Sekondari kadhalika kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowawezesha kujitegemea.
Aidha, ameagiza Bodi husika kuhakikisha viziwi wanapewa elimu ya uchumi na uwezeshaji ili kuweza kujikwamua kiuchumi kadhalika na kuandaa ripoti ya namna gani mmeweza kutoa matokeo chanya katika kusimamia viziwi kupata masilahi yao ikiwemo kufanya ujasiriamali na kunufaika na mikopo mbalimbali inayotolewa na Halmashauri na Wizara ambayo ni ya makundi maalum.
Sambamba amewaasa Wakalimani kuwa na maadili ya kutunza siri za viziwi kwa kuwadhalilisha kwa kutoa siri zao za ndani kwa watu wasiohusika hali inayowafanya wajisikie vibaya kwa kuona wamedhalilishwa utu wao kutokaana na madhaifu yao.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan inawatambua na kuwajali kwa kuwapa kipaumbele viziwi kwa kuanzisha vituo mbalimbali vya kuwahudumia ikiwemo Vituo 176 nchi nzima,Vifaa vya kujifunzia kadhalika imeweka mikakati madhubuti ya kushughulikia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi), ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa elimu jumuishi na huduma za afya rafiki kwa viziwi.
Kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Wizara ya Elimu, serikali imeongeza ajira kwa wakalimani wa lugha ya alama, kuwezesha upatikanaji wa vifaa saidizi kama vile vifaa vya usikivu na kuboresha miundombinu ya shule ili iwe rafiki kwa wanafunzi viziwi.
Aidha, serikali imeendelea kushirikiana na mashirika ya kiraia katika kutoa elimu ya lugha ya alama kwa watumishi wa umma ili kuongeza ushirikishwaji wa viziwi katika huduma za kijamii na shughuli za kitaifa. Mikakati hii inaendana na dhamira ya serikali ya kuhakikisha usawa, ujumuishaji na ustawi wa makundi maalum katika maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment