
Viongozi na wataalamu wa afya wametakiwa kusimamia kwa umakini utekelezaji wa Mradi Endelevu wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSSP) ili kufanikisha lengo la kuwa na mkoa wenye viwango vya juu vya usafi ifikapo mwaka 2025.
Akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo leo (15 Agosti 2025), Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Singida Ndg.Nesphory Bwana, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, amesema mpango huo, unaotekelezwa kwa mfumo wa Malipo kwa Ufanisi (Result Based Financing), umewezesha mkoa kupokea zaidi ya shilingi bilioni 6.42 katika kipindi cha miaka mitano, na kuboresha miundombinu ya maji na usafi katika vituo 154 vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Victorina Ludovick amesema miradi ya usafi wa mazingira na uboreshaji wa miundombinu ya maji imekuwa chanzo muhimu cha mapato kwa mkoa, na kufafanua kuwa mwaka 2021 ulipokelewa mtaji wa kuanzia wa shilingi milioni 262.87, lakini hadi kufikia mwaka wa fedha 2024/2025 zaidi ya shilingi bilioni 6 zimepokelewa. Fedha hizo zimetumika kujenga vyoo, vichomea taka, kuboresha maeneo ya huduma za mama na mtoto na miundombinu ya maji safi na salama.
Aidha, amesema kikao hicho pia kinajadili ushirikiano na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ukaguzi na usajili wa maeneo ya biashara, ambapo asilimia 40 ya mapato yatabaki halmashauri na asilimia 10 kuingia mkoani, hatua ambayo itaimarisha mapato.
Naye Afisa Afya Mkoa wa Singida, Bw. Mgeta Sebastian, ameeleza kuwa huduma za WASH zimeboreshwa na kuwafikia makundi maalumu, hususan wenye ulemavu na afya ya mama na mtoto huku Idadi ya kaya zenye vyoo bora ikiongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2020 hadi 75.9 mwaka 2025, kadhalika vifaa vya kunawia mikono vikiongezeka kutoka asilimia 16 hadi 46 katika kipindi hicho. Amesema pia uelewa wa wananchi kuhusu usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo jumuishi umeimarika.
Bw. Mgeta ameongeza kuwa mkoa umefanikisha ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi, kuhamasisha jamii kutumia vyoo bora, na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kijamii na kidini katika kutekeleza sheria za mazingira.
Kikao hicho kimeazimia kuendelea kusimamia kwa ufanisi miradi ya maji na usafi wa mazingira, ili Singida ibaki kinara wa afya bora na mazingira safi nchini.
Kwa undani zaidi wa yaliyojiri katika kikao hicho tafadhali fatilia kiungo kifuatacho kuona Video ya kikao hicho
👇👇👇👇👇
No comments:
Post a Comment