Sunday, April 21, 2024

RC SINGIDA AAGIZA KUKAMATWA KWA WANAFUNZI WALIOPATA MIMBA MASHULENI ILI WAWAJIBISHWE KISHERIA WAKIWEMO WAZAZI.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, ameagiza kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wanafunzi wa kike waliopata mimba wakiwa shuleni wakiwemo wazazi kama hatua ya kukomesha tatizo hilo ambayo limeonekana kuwa ni kero kubwa katika maendeleo ya sekta elimu mkoani humo.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakati anakagua ujenzi wa miradi ya maendeleo pamoja na kuzugumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kijiji Songambele mjini Itigi ili kutatua kero zinazowakabili.

Dendego, amesema ili kukomesha tatizo hilo yeye ataanza kukamata kwanza msichana aliyepata mimba na baadaye mvulana ambaye atakuwa mtuhumiwa namba mbili kama hatua ya kukomesha vitendo vya mimba kwa wanafunzi.

“Nikikuta msichana umepata mimba wewe utakuwa mshtakiwa namba Moja na wewe ndio utakayeenda jela bila huruma na tumbo lako utajifungulia huko huko kwa sababu mna tabia ya ukipata mimba tunaenda kukimbizana na mtoto wa kiume si sawa wote mlishirikiana kwa hiyo yeye atakuwa mstakiwa namba mbili na msichana atakuwa mstakiwa namba Moja,” Amesisitiza RC Halima Dendego.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (wa kati waliokaa) akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitaraka iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba za Walimu.

Kuhusu wanafunzi 4,000 kutoripoti shuleni mkoani Singida hadi sasa, Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, ametoa muda wa mwezi Mmoja kwa Makatibu Tarafa na Maafisa Watendaji wa Vijiji na Kata wahakikishe wanawasaka wanafunzi hao popote walipo na kuwarudisha shuleni vinginevyo watakiona cha moto.

Amesema itakuwa jambo la aibu kwa Serikali kujenga shule kwa gharama kubwa huku wanafunzi wanaotakiwa kusoma kwenye shule hizo hawapo shuleni na kusisitiza kuwa hatakubali hata kidogo aibu hiyo imkute na ni lazima wanafunzi hao wasakwe popote walipo ili warudishwe shuleni wakasome.

RC Dengedo, ameagiza kupatiwa taarifa zote za wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ambao hawajaripoti shuleni mpaka sasa hata kama wamehama na shule walipohamia ili aweze kufuatilia kama ni kweli yupo kwenye shule hiyo au ni uongo. 

Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitaraka iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba za Walimu.

Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa mfano kwa wazazi na jamii nzima na kuachana na mambo yanaenda kinyume cha maadili ya Kitanzania.

Dkt. Fatuma Mganga, amesema kuwa kama wanafunzi watasoma kwa bidii hadi Vyuo Vikuu watakuwa na faida kubwa sio tu kwa familia zao bali kwa jamii nzima na Taifa kwa ujumla kwa sababu Serikali imeboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akisikiliza kero mbalimba za wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kijiji cha Songambele.

Mmoja wa mwananchi akitoa kero yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego alipofanya mkutano wa hadhara katika halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mmoja wa Mwananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Bw. Mussa Shaban Kambi, (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa kibali kuhusu kumalizika kwa kesi yake inayomkabili ili aweze kupatiwa haki yake. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, akijibu maswali mbalimbali ya wananchi kuhusu kero zao zinazowakabili  kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero na kuzitatua.

Mkuu wa Mkoa wa Singida akishiriki ujenzi wa nyumba za Walimu katika shule ya Sekondari Kitaraka Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakati alipofanya ziara ya siku mbili kukagua miradi ya maendeleo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, akishiriki ujenzi wa nyumba za Walimu katika shule ya Sekondari Kitaraka Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakati wa ziara ya siku mbili ya Mkuu wa Mkoa huo kukagua miradi ya maendeleo.

Muonekano wa Jengo la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Itigi

Mkuu wa Mkoa akisisitiza jamo wakati wa ziara hiyo.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya Shule ya Sekondari ya Kitaraka iliyopo katika halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, (mwenye kilemba) akifuatilia taarifa ya ujenzi wa nyumba ya walimu inayojengwa katika shule ya Sekondari Kitaraka.

No comments:

Post a Comment