Thursday, April 18, 2024

RAS SINGIDA AAGIZA WAATHIRIKA WALIOACHA KUTUMIA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI WATAFUTWE

Serikali Mkoani Singida imeaagiza Waganga Wakuu wa Wilaya na Wadau wengine wa Afya kuwatafuta na kuwarejesha katika matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI kwa waathirika 857 ambao wameacha kutumia dawa hizo katika Halmashauri Tatu (3) za Itigi, Ikungi na Singida.

Agizo hilo limetolewa (tarehe Aprili 18, 2024) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga wakati anafungua kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa USAID AFYA YANGU ambao unatekelezwa Mkoani humo.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa ameonyesha kutoridhishwa na idadi hiyo kubwa ya watu wanaotuma dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kuacha kutumia dawa hizo na amesisitiza kuwekwa kwa mikakati na mipango madhubuti itakayosaidia kurejesha kundi hilo katika matumizi ya dawa hizo haraka iwezekanavyo.

Amesema kuna umuhimu wa kutengeneza mahusiano mazuri kati na watoa huduma na wateja wao ikiwemo kuwapigia simu pindi wanapoona mteja wao hafiki kuchukua dawa ili kujua sababu ambazo zinamfanya asiende kuchukua dawa hizo ili kuona namna bora ya kumsaidia.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick, ametaja sababu zinazopelekea idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI mkoani humo kuacha kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo kuwa ni waathirika hao kuhama na kwenda maeneo mengine na umbali kutoka kwenye makazi yao hadi kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.

Ludovick amesema mpango uliopo kwa sasa ni kuhakikisha watumiaji hao wa dawa za kufubaza virusi hivyo wanatafutwa popote walipo na kuwapa ushauri nasaha kuhusu umuhimu wa matumizi ya dawa hizo kwa ajili ya afya zao.

Naye, Meneja Mradi wa USAID AFYA YANGU mkoani Singida, Said Mgeleka, amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa katika Mkoa huo ambapo umeweza kusaidia kuibua watu zaidi ya 700 walioathirika na virusi vya UKIMWI kila baada ya miezi Mitatu na kuwaazishia dawa haraka mara baada ya kugundulika.

Mradi wa USAID AFYA YANGU unatekelezwa katika Mikoa Sita (6) ya Tanzania Bara ambayo ni SINGIDA, DODOMA, MANYARA, TABORA, ARUSHA na KILIMANJARO.












No comments:

Post a Comment