Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza katika baraza la biashara la mkoa kwenye
ukumbi wa ofisi yake. Wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Singida Kitila
Mkumbo na kushoto ni katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida amefuata
nyayo za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli kwa
kuzuia mchanga wa dhahabu unaopatikana mkoani hapa kutosafirishwa nje ya nchi kwa
kitendo chake cha kuzuia mchanga wa dhahabu kutoka nje ya mkoa.
Akizungumza katika kikao
cha baraza la biashara la Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi
amesema wadau kutoka sekta binafsi na ya umma waliohudhuria kikao
hicho wamekubaliana kwa kauli moja kupiga marufuku mchanga wenye dhahabu
kusafirishwa nje ya mkoa kwa ajili ya uchenjuaji.
Dkt. Nchimbi amesema ili
kuendana na kasi ya Mhe rais ya kuwaletea maendeleo watanzania wanyonge,
mchanga huo wa dhahabu uchenjuliwe hapa hapa mkoani Singida ili malipo ya mrabaha
yaongezeke na kukuza pato na uchumi wa mkoa.
Mmoja wa wadau wa sekta
binafsi Angasen Nkya amesema kuwa kwa muda mrefu baadhi ya wachimbaji madini
wamekuwa wakisafirisha mchanga wenye madini nje ya mkoa, badala ya kuuchenjua
hapa mkoani.
“Mchanga wenye madini
kutoka machimbo mbalimbali mkoani hapa yakiwemo ya kijiji cha Mahintiri wilaya
ya Ikungi umekuwa ukisafirishwa kupelekwa mikoa mingine ukiwemo mkoa wa Mwanza.
Kitendo hichi kinapunguza kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri na serikali
ya mkoa, yatokanayo na tozo la mrabaha”,amefafanua Nkya.
Aidha Dkt. Rehema Nchimbi amewaagiza wakuu wa wilaya na wakuu wa
vituo vya polisi vya wilaya zote mkoani hapa kuhakikisha mchanga wenye madini
hautoki nje ya mkoa na mchimbaji atakayekiuka agizo hilo achukuliwe hatua
stahiki.
Naye Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu amesema utaratibu
uliopo wa leseni za uchimbaji madini kutolewa na wizara bila kushirikisha
mamlaka za wilaya unawanyima uhuru wa kusimamia shughuli za uchimbaji madini
katika maeneo yao kwa ufanisi.
“Wizara ya nishati na madini inachofanya ni kuipa ofisi ya mkuu wa
wilaya nakala ya barua ikielekeza kampuni fulani imepewa leseni ya kuchimba
madini kwenye eneo la wilaya yake. Migogoro ikizuka ndipo mkuu wa wilaya
anapoonekana ana umuhimu katika shughuli za uchimbaji madini", amesema
Mtaturu.
Ameongeza kuwa ni jambo njema endapo wizara ya nishati na madini ikashirikisha
uongozi wa wilaya kuanzia shughuli za utafiti na uchimbaji madini
mapema kabisa ili kurahisisha ufuatiliaji na kuzuia uwezekano wa ktuokea
migogoro au uvamizi wa maeneo ya shughuli za madini.
Awali Dkt. Nchimbi amesema baraza la biashara la mkoa sio sehemu
ya kupeleka malalamiko na kuikosoa serikli tu bila ya kuwa na mbinu mbadala za
kushauri na kutoa maoendekezo yenye lengo la kukuza sekta ya bishara kwa mkoa
wa Singida.
Ameongeza kuwa baraza hilo liimarishwe zaidi ili liweze kutengeza
umoja kati ya sekta ya umma na binafsi huku kamati mbalimbali zikipendekezwa
kuundwa ili zitatue kero na kubuni mbinu za kuboresha biashara Mkoani Singida.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewataarifu
wafanyabiashara na wananchi wote wa Mkoa wa Singida kuwa bomba kubwa la mafuta
kutoka Nchini Uganda hadi bandari ya Tanga litapitia katika baadhi ya vijiji
vya wilaya ya Iramba, Singida na Ikungi.
Dkt. Nchimbi amesema kila mahali bomba hilo litakapopita viongozi
na wananchi kwa ujumla watoe ushirikiano wa karibu ili kufanikisha ujenzi huo
na pia kuzitumia fursa zilizopo kwa uaminifu, uadilifu na ubunifu mkubwa.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha baraza la
biashara la mkoa wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye kikao hicho kilichofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu akisisitiza jambo wakati akichangia mada
kwenye kikao cha baraza la biashara la Mkoa wa Singida.
Mfanyabiashara Mkoani Singida Mzee Aklan akichangia mada kwenye kikao cha baraza la biashara la Mkoa wa Singida.
No comments:
Post a Comment