Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga ametoa wito kwa walimu wa shule za msingi kuongeza ubunifu katika ufundishaji ili kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba.
Akiendelea kuzungumza, Katibu Tawala Dkt.Mganga amesisitiza umuhimu wa walimu kuhakikisha wanafunzi wanakuwa nadhifu na wenye usafi muda wote. Amesema suala la usafi ni sehemu ya malezi na maandalizi ya mwanafunzi kujiandaa na hatua inayofuata ya elimu. Kadhalika, amewataka wanafunzi kuheshimu muda wa kufika shuleni na kuwatii walimu wao, sambamba na kuhakikisha mazingira ya shule na madarasa yanabaki kuwa safi ili kuweka msingi wa nidhamu na utendaji bora.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida akapata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi hao na kuwataka kuongeza bidii katika masomo yao. Ameahidi kuanzisha mbinu shirikishi na rafiki kwa walimu ambazo zinalenga kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kuanzia mwaka ujao. Aidha, amesema kuwa mitihani ya mazoezi ya kila mwezi itaanza kutolewa kuanzia Januari, na wanafunzi watakaofanya vizuri watazawadiwa ili kuongeza ari ya kujifunza na ushindani chanya miongoni mwao.
Kwa upande wa wanafunzi, Lucas Mwagoko ameonesha kujawa na hamasa na kuahidi kusoma kwa bidii ili kufaulu kwa kiwango cha juu katika mtihani wao wa taifa wa darasa la saba mwaka 2026. Amesema hotuba na maagizo yaliyotolewa yamewapa motisha ya kufanya kazi kwa bidii na kujiandaa mapema.
Ziara hiyo pia ilihusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayoendelezwa na Serikali Kuu katika Shule ya Msingi Sophia, ikiwemo ujenzi wa madarasa matatu, nyumba ya mwalimu na matundu 38 ya vyoo. Utekelezaji wa miradi hiyo unaelezwa kuwa sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha miundombinu ya elimu na kuweka mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.
Katika matokeo ya darasa la saba kitaifa mwaka 2025 Mkoa wa Singida umepata wastani wa 81.
Kupitia maboresho hayo, Serikali inaendelea kuwaandaa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa kuwajengea mazingira salama na rafiki ya kujifunzia. Hii inajumuisha ujenzi wa madarasa mapya, mabweni na maktaba, upatikanaji wa vitabu vya kutosha, vifaa vya maabara, TEHAMA, na kuongeza nguvu kazi ya walimu. Hatua hizo zinahakikisha kuwa wanafunzi wanapofika sekondari wanakutana na mazingira yaliyoboreshwa yanayowawezesha kusoma kwa ufanisi na kufikia malengo yao ya kitaaluma.











No comments:
Post a Comment