Thursday, November 27, 2025

UKAGUZI WA MIRADI YA MAENDELEO WAFICHUA HATUA ZA UTEKELEZAJI

 Timu ya ukaguzi wa miradi ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt.Fatuma Mganga imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida leo tarehe 27 Novemba 2025, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, afya na miundombinu, pamoja na thamani ya fedha katika matumizi yake.

Katika Shule ya Msingi Ghata, wajumbe walikagua mradi wa ujenzi wa choo chenye matundu 14, uliogharimu Tsh 23,800,000 kutoka LANES GPE. Mradi huo unahusisha matundu sita ya wavulana yenye mahitaji maalum na matundu nane kwa wasichana. Hadi sasa kiasi cha Tsh 21,800,281 kimeshatumika na ujenzi upo katika hatua ya kupaua huku kazi ikiendelea.

Ziara hiyo pia ilifika kwenye mradi wa jengo la kuhifadhia maiti (mortuary) pamoja na barabara za watembea kwa miguu. Mradi huo ulipokea Tsh 300,000,000 katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa mortuary na walkways zenye jumla ya mita 240 na upana wa mita 2. Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 42 ya kukamilika.

Katika Kituo cha Afya Kinyagigi, ukaguzi umeonyesha hatua za awali za upanuzi wa kituo hicho baada ya kupokea Tsh 250,000,000 mnamo 30 Juni 2025. Fedha hizo zinahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), ukarabati wa nyumba ya watumishi, ujenzi wa jengo la maabara, vyoo matundu manane pamoja na kichomea taka (ash pit na placenta pit). Mpaka sasa kiasi cha Tsh 39,464,900 kimetumika.


Katika Shule ya Msingi Sokoine, kamati ilikagua ujenzi wa nyumba mbili ndani ya jengo moja, zilizofadhiliwa kwa Tsh 95,000,000 kutoka LANES GPE. Mradi huo, ambao umefikia asilimia 85 ya kukamilika baada ya kutumia Tsh 81,000,000, unatarajiwa kupunguza changamoto kwa walimu wanaotembea umbali mrefu kutoka Msange.

Ukaguzi ulihitimishwa katika Shule ya Sekondari Maghojoa ambako ujenzi wa mabweni mawili unaendelea. Mradi huo ulipokea Tsh 250,000,000 kupitia mpango wa EP4R II tarehe 7 Machi 2025 kwa ajili ya mabweni yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 90 kila moja. Hadi sasa Tsh 212,027,848.60 zimetumika na mradi unatarajiwa kupunguza adha ya wanafunzi wanaotembea hadi kilomita saba kufika shuleni.

Kwa ujumla, ukaguzi umeonyesha hatua za maendeleo katika utekelezaji wa miradi huku baadhi zikiwa katika hatua za kati na nyingine zikiwa karibu kukamilika, lengo likiwa kuboresha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Singida.






No comments:

Post a Comment