Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameagiza viongozi wa Halmashauri kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa Soko jipya la Vitunguu lililopo Kititimo, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa viwango vya juu.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika eneo jipya la ujenzi wa soko hilo, Mhe. Dendego amesema Serikali ina dhamira njema ya kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na kuhakikisha Singida inakuwa kitovu cha biashara ya vitunguu nchini.
“Singida tunakwenda kipindua meza, tunakwenda kuweka historia ya kipekee kwa mradi huu mkubwa na wa kipekee. Hii ni moja ya sababu ya kwenda kuuweka mkoa wa Singida kwenye ramani ya kuwa Jiji la Singida. Na hili linawezekana kwa utekelezaji wa miradi hii mikubwa. Tutegemee mwezi Septemba 2026 kukata keki ya mafanikio baada ya kukamilika kwa mradi huu wa TACTIC,” amesema Mhe. Dendego.
Kadhalika, amemtaka mkandarasi kuhakikisha maeneo muhimu yanazingatiwa katika ujenzi wa soko hilo ikiwemo maeneo ya zahanati, michezo, mapumziko, kumbi za mikutano pamoja na maeneo ya sekta binafsi kuwekeza katika huduma za kifedha. Amesisitiza pia kazi kufanyika kwa ubora ili gharama kubwa za ujenzi ziendane na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, aliwataka wajumbe wa kikao hicho kufikisha salamu za Serikali kwa wananchi na wafanyabiashara wa Soko la Vitunguu juu ya nia njema ya kuhamishia soko hilo maeneo mapya. Amesema eneo hilo jipya litakuwa rafiki zaidi kwa wafanyabiashara na litakidhi idadi kubwa ya wajasiriamali kuliko soko la sasa, hivyo kuongeza faida maradufu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Vitunguu-Misuna, Bw. Iddi Mwanja, amesema wafanyabiashara wamepokea kwa mikono miwili na kwa furaha kubwa mradi wa soko jipya kwa kuwa utawanufaisha kwa kiasi kikubwa sambamba na kufanya kazi zao kwa uhuru katika mazingira bora na rafiki kwa wote.
“Serikali yetu tunaiamini, tuiache ifanye kazi yake. Tutafuata utaratibu tunaopewa kwa sababu ina nia njema kwetu sisi wananchi,” amesema Bw. Mwanja.
Naye Katibu wa Soko la Vitunguu, Bw. Mshujaa Salum Mwacha, amesema hawana hofu kwani viongozi wamekuwa wakiwasikiliza na kuwashirikisha vizuri katika kila hatua ya maandalizi ya mradi huo. Ameongeza kuwa wamefurahia kuona soko jipya limewapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalum sambamba na akinamama wanaonyonyesha.
Mkandarasi anayehusika na ujenzi huo ameahidi kuhakikisha ujenzi unakuwa wa viwango vya juu na unakamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa wananchi wa Singida wajiandae kupokea soko zuri la kisasa lenye mazingira rafiki kwa kazi zao za kila siku.Amesema kuwa ukubwa wa soko hilo ni mita za mraba 32,547.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Katibu Tawala wa Wilaya, Wajumbe wa Soko la Vitunguu, Afisa Mazingira, Afisa Maendeleo ya Jamii, Mtaalam wa Ardhi, wataalam kutoka TARURA, wakandarasi na wadau wengine wa maendeleo.
Mradi huu wa ujenzi wa Soko jipya la Vitunguu unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya biashara mkoani Singida kwa kuboresha mazingira ya wafanyabiashara, kuongeza mapato ya Serikali, kutoa ajira kwa wananchi, pamoja na kuongeza thamani ya zao la vitunguu linalolimwa kwa wingi katika mkoa huo. Soko hilo pia litakuwa na miundombinu rafiki kwa watu wote, likiwa na huduma muhimu kama zahanati, maeneo ya mapumziko, michezo na huduma za kifedha, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Singida na kuchangia utekelezaji wa mpango wa kuifanya Singida kuwa Jiji la kisasa.
No comments:
Post a Comment