
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amefanya ziara katika Halmashauri za Wilaya ya Iramba na Mkalama kwa ajili ya kukagua maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dendego amekutana na viongozi mbalimbali wa Halmashauri hizo wakiwemo Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Wasimamizi wa Uchaguzi, pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, ili kujiridhisha na hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya uchaguzi huo.
Kadhalika,lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu yanakwenda vizuri na kwamba wananchi wote wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo la kikatiba kwa amani, utulivu na uwazi ikiwemo kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kupiga kura ni rafiki kwa wananchi na yanafikika bila changamoto,kuhakikisha uwepo wa vifaa vyote muhimu vinavyotumika wakati wa kupigia kura mfano masanduku ya kupigia kura,wino na wasimamizi wa uchaguzi kufahamu utayari na changamoto kama zipo ili kufanyiwa kazi na mengineyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dendego alisema:“Tunataka kuona Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unafanyika katika hali ya amani na utulivu. Viongozi wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi, wote tushirikiane kuhakikisha Singida inakuwa mfano wa uadilifu na utulivu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.”
Ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Singida imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu katika wilaya zote, halmashauri zote na mpaka ngazi ya kata, huku akihimiza viongozi na watendaji kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kutoa elimu ya uraia na umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Singida kuendelea kudumisha mshikamano na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Kadhalika Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga alifanya ziara yenye lengo sawa na hilo katika Wilaya ya Manyoni ambapo pia aliambatana na Viongozi wa Idara mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika nchini mnamo Oktoba 29,2025 ambapo utahusisha uchaguzi katika ngazi ya Rais,Wabunge na Madiwani.
No comments:
Post a Comment