Saturday, October 25, 2025

RC DENDEGO ATETA NA WATUMISHI USHIRIKI UCHAGUZI


 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameongoza kikao na wakuu wa taasisi pamoja na watumishi wote wa Serikali wa Mkoa wa Singida leo, Oktoba 25, 2025, chenye lengo la kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ijayo, Oktoba 29, 2025.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Dendego amewakumbusha watumishi na wakuu wa taasisi kuzingatia maelekezo ya kisera yaliyotolewa kuelekea Uchaguzi Mkuu, 

Akiwakumbusha maelekezo yake ya kisera kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewataka watumishi wote wa umma kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho halali vya wapigakura na kufika mapema katika vituo vyao vya kupigia kura kabla ya muda wa kufungwa. Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kuwa mfano wa utii kwa sheria kwa kufuata kikamilifu maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamoja na viongozi wa usalama, ili kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na uwazi.

Aidha, amekemea vikali vitendo vinavyoweza kuashiria upendeleo wa kisiasa, akiwataka watumishi kuepuka kuvaa mavazi au kubeba nembo za vyama vya siasa, pamoja na kujiepusha na matamshi, maandiko au mienendo yoyote inayoweza kuchochea chuki, vurugu au ubaguzi katika jamii. Ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji, bila kuegemea upande wowote wa kisiasa, ili kudumisha heshima ya utumishi wa umma na kuonesha mfano bora wa uadilifu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka watumishi wote kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, na badala yake kutumia mitandao hiyo kwa elimu, uhamasishaji chanya na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Aidha, Dkt. Mganga ametoa wito wa kujilinda binafsi na kulinda familia, kwa kuepuka kutembea katika maeneo hatarishi hasa nyakati za usiku, na kufanya majukumu yao mapema ili kuepuka usumbufu wowote siku za uchaguzi.

Nao wakuu wa taasisi mbalimbali mkoani Singida, wameahidi kujitokeza mapema ifikapo saa moja asubuhi siku ya uchaguzi, kuhakikisha wanatekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura, na kuwa mfano bora kwa watumishi na wananchi kwa ujumla.








No comments:

Post a Comment