Sekretarieti ya Mkoa wa Singida imepokea zaidi ya shilingi bilioni tatu kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya viongozi wa serikali mkoani humo.
Fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuboresha miundombinu ya ofisi na makazi ya viongozi katika ngazi za mikoa na wilaya. Kupitia mpango huo, ofisi tatu za wakuu wa wilaya zitajengwa katika Wilaya za Iramba, Manyoni na Singida, ambapo kila moja imetengewa bajeti ya shilingi bilioni moja (1,000,000,000).
Aidha, serikali imetenga kiasi cha takribani shilingi milioni 454 kwa kila nyumba ya makazi ya Wakuu wa Wilaya za Manyoni na Iramba, sambamba na bajeti ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida.
Akizungumza leo Oktoba 27, 2025, wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Iramba, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego amefika katika eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba na nyumba ya makazi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, ambapo alijadiliana na viongozi wa eneo hilo kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo.
Kupatikana kwa majengo hayo mapya kutaboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kazi na utendaji wa viongozi wa serikali, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi, pamoja na kuimarisha usimamizi wa shughuli za maendeleo katika wilaya na mkoa kwa ujumla.
Vilevile, ujenzi huo utachochea fursa za ajira za muda mfupi kwa wananchi wa maeneo husika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Singida.








No comments:
Post a Comment