Saturday, November 29, 2025

WAHITIMU WAHIMIZWA KUJITUNZA NA KUJILINDA WATAKAPOREJEA MAJUMBANI


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewaasa vijana wahitimu wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu (Saba Saba) kujitunza na kufuata maadili watakaporejea mitaani baada ya kumaliza masomo yao, akisisitiza kuwa ujana ni rasilimali isiyorudi na ukiupoteza huathiri maisha ya baadaye.

Akizungumza wakati wa mahafali ya chuo hicho, Mhe. Dendego aliwataka vijana kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na ngono zembe, akiwakumbusha msemo wa “Kula nanasi kwataka nafasi”, akimaanisha umuhimu wa kusubiri muda muafaka kabla ya kuingia katika mahusiano ili kuepuka mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa.

Aidha, aliwaelekeza wakurugenzi, maafisa ustawi na maendeleo ya jamii kuhakikisha vijana wanaunganishwa katika vikundi na kupewa mitaji ili kuwawezesha kuanzisha shughuli za uzalishaji mali badala ya kubaki mitaani bila ajira. Alitoa wito kwa waajiri kuacha kuwaona vijana kama dhaifu, badala yake wawapatie ushirikiano na fursa za kazi.

Mhe. Dendego pia aliwasisitiza vijana kuepuka uharibifu wa rasilimali za taifa kama njia ya kutafuta suluhu ya changamoto zao, bali kuzitumia kwa manufaa yao. Aliwahimiza wahitimu kuwasilisha mawazo ya miradi yao ili kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa makundi maalumu, hatua itakayowawezesha kuanzisha biashara na kukuza uchumi wao.


Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bi. Yasinta Alute, aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, alisema kupungua kwa changamoto za afya ya akili miongoni mwa vijana kunatarajiwa kutokana na kuongezeka kwa uelewa na elimu pamoja na fursa za ajira zitokanazo na ujuzi wanaoupata vyuoni. Alisema kipato kitakachotokana na ujuzi huo kitawasaidia vijana kupata utulivu wa fikra na kupunguza msongo wa mawazo.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu wa Mkoa, Bi. Sarah Mkumbo ambaye ni Afiaa elimu ya watu wazima,aliwahakikishia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira rafiki ya kujifunzia, ikiwemo miundombinu wezeshi ili kuwarahisishia elimu. Aliwaomba kuwa mabalozi kwa vijana wengine wenye ulemavu ili wajitokeze kujiunga na mafunzo ya ufundi.

Naye Mkuu wa Chuo hicho, Bi. Fatuma Malenga, alisema chuo kimepata mafanikio makubwa kupitia programu ya wanagenzi ambayo imeongeza mwamko kwa vijana kujifunza fani za ufundi. Hata hivyo alitaja changamoto zinazokikabili chuo hicho kuwa ni pamoja na kuibiwa kwa uzio wa chuo, ukosefu wa ukumbi wa mihadhara na baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudumiwa ipasavyo kutokana na hali duni ya wazazi wao.






No comments:

Post a Comment