Thursday, April 20, 2017

SINGIDA YAANZISHA MADAWATI YA SEKTA BINAFSI KILA HALMASHAURI.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akifungua mafunzo ya wawezeshaji   wananchi uchumi wa kwa mikoa mitano ya kanda ya kati yaliyofanyika mjini Singida .


Mkoa wa Singida umeanzisha madawati ya sekta binafsi katika halmashauri zake saba za Mkoa ili kuratibu changamoto na fursa zilizopo katika kuboresha sekta binafsi kwakuwa zimekuwa zikichangia uchumi wa taifa kwa kiasi kikubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya viongozi na wawezeshaji wa baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kanda ya kati ikijumuisha mikoa ya Singida, Dodoma, Shinyanga, Simiyu na Shinyanga.

Dkt. Nchimbi amesema sekta binafsi zimekuwa zikitoa huduma kwa wananchi na kuongeza uchumi wa taifa hivyo serikali inapaswa kuwezesha uboreshaji wa mazingira ili zifanye kazi kwa ufanisi.

Aidha amesema katika kusaidia sekta binafsi zilizopo mkoani Singida, halmashauri zote zimekubaliana kutangaza bidhaa na huduma zitolewazo na sekta hizo ili zipate fursa ya kujulikana na watanzania pamoja huduma na fursa za uwekezaji kwa kila halmashauri.

Amesema Mkoa wa Singida una fursa nyingi za uwekezaji katika kilimo, biashara, madini na utalii na mkoa wa Singida si masikini wala kame kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidhani.

“Singida hakuna ukame, mahindi yana stawi vizuri, alizeti tunastawisha kwa wingi sana, vitunguu vizuri vinastawi kwa wingi, tuna fuga kuku wazuri wa kienyeji ambao hawaishi na husambazwa kote nchini, tuna madini ya dhahabu na aluminium, mtu akisema Singida ni kame na masikini nadhani anakosea kabisa” ameongeza Dkt. Nchimbi.

Akizungumza kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi Dkt. Nchimbi amesema baraza hilo litafanikiwa endapo uwezeshaji utajikita zaidi katika kutoa elimu na kubadilisha wananchi kifikra ili waendane na kasi ya kuchapa kazi na kuwa wabunifu.

Naye mwenyekiti wa baraza la uwezeshaji Taifa, Dkt. John Jingu amesema lengo la kuanzishwa kwa baraza hilo ni kuwezesha wananchi wote wanashiriki kikamilifu katika kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

Dkt. Jingu amesema baraza litajikita katika kuboresha kilimo hasa cha umwagiliaji na upatikanaji wa masoko ya nafaka zinazozalishwa na wakulima na kuboresha ufugaji ili uwe wa kisasa.

Mafunzo kwa viongozi na wawezeshaji wananchi kiuchumi kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Manyara, Shinyanga na Geita yamefanyika Mjini Singida katika ukumbi wa Veta ambapo wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maafisa wawezeshaji kutoka mikoa hiyo wameshiriki. 

Mwenyekiti wa baraza la uwezeshaji Taifa, Dkt. John Jingu akizungumza na washiriki wa mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kanda ya kati yalifanyika Mkoani Singida.

Afisa kutoka baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi Bi Beng'i Issa akisoma taarifa ya baraza la taia la uwezeshaji wananchi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Kufungua mafunzo kwa wawezeshaji na viongozi wa mikoa mitano ya kanda ya kati.
  
Baadhi ya Viongozi na wawezeshaji wakifuatilia kwa umakini mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa wawezeshaji na viongozi wa mikoa mitano ya kanda ya kati.

No comments:

Post a Comment