Mkulima wa Alizeti Mkoa wa Singida akipalilia zao hilo, mkulima huyu amefuata ushauri wa kitaalamu wa kupanda kwa mistari, kuweka mbolea na kutumia mbegu mpya ya record ambayo huzalisha kwa wingi.
Afisa kilimo na Mratibu wa MIVARF Mkoa wa Singida akimsikiliza mkulima wa Alizeti Mkoa wa Singida akipalilia zao hilo, mkulima huyu
amefuata ushauri wa kitaalamu wa kupanda kwa mistari, kuweka mbolea na
kutumia mbegu mpya ya record ambayo huzalisha kwa wingi.
Wakulima wa alizeti
Mkoani Singida wameazimia kuwa wazalishaji namba moja nchini wa alizeti kwa wingi
na ubora wa hali ya juu kutokana na kutumia mbinu bora na za kisasa huku
wakiachana na kilimo cha mazoea kilichowapa matokeo kidogo na yasiyo na ubora.
Wakulima wa Wilaya
tatu za Iramba, Manyoni na Singida wamefikia uamuzi huo katika vikao kati yao
na kamati ya ufuatiliaji wa progamu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Masoko,
Uongezaji wa thamani ya mazao na Huduma za kifedha vijijini (MIVARF) iliyokuwa
ikifanya tahmini ya mradi huo kwa kutembelea mashamba na kuzungumza na wakulima
hao.
Mwenyekiti wa Kikundi
cha Mwangaza cha wakulima wa Alizeti kata ya Sanjaranda Wilayani Manyoni Bi.
Janeth Emmanuel amesema, mradi wa MIVARF umewahamasisha kutumia mbegu ya
alizeti ya kisasa aina ya record ambayo huzalisha wastani wa gunia 12 mpaka 16
kwa ekari moja wakati mbegu ya zamani ambayo walikuwa wakiitumia ya zebra
imekuwa ikizalisha gunia mbili mpaka nne kwa ekari moja.
Bi Janeth amesema
kutokana na wakulima wengi kuhamasika kutumia mbegu mpya ya record na kufuata
elimu waliyopewa na MIVARF, Mkoa wa Singida utazalisha alizeti nyingi na bora
kwa ajili ya viwanda vya ndani na nje ya Mkoa.
Amesema wakulima wa
alizeti walikua hawafuati ushauri wa kupanda zao hilo kwa mistari, kuacha
nafasi pamoja na kuweka mbolea ambapo awali walidhani alizeti haihitaji kuwekewa
mbolea kitu ambacho sio sahihi na hivyo kupelekea mkulima kutumia eneo kubwa na
kuzalisha kidogo.
Bi. Janeth ameongeza
kuwa kutokana na matarajio ya kuvuna alizeti nyingi elimu zaidi juu ya
uongezaji wa thamani wa alizeti itolewe kwa wakulima ili waweze kupata faida
kubwa tofauti na awali ambapo wamekuwa wakimwaga mashudu ambayo huzalisha kiwi
na mkaa na kuuza alizeti ghafi badala ya mafuta.
Naye Mtoa huduma wa
MIVARF Wilaya ya Manyoni Anthony Mtu amesema mradi huo umewafikia wakulima elfu
mbili katika kata ya Sanjarada huku wakianzisha mashamba darasa 12 ya zao la
alizeti yenye ukubwa wa ekari 24 huku matarajio ya mavuno kwa mashamba darasa
yakiwa ni magunia 288.
Mtu amesema wakulima
wamehamasika kutumia mbegu ya record baada ya kuelimishwa kuwa mbegu hiyo, inatumia
maji kwa ufanisi, inatoa mavuno mengi na haishambuliwi na magonjwa kwa urahisi.
Kwa upande wake Afisa
Kilimo na Mratibu wa MIVARF Mkoa wa Singida Lucas Mkuki amesema mradi huo
umeanza kutekelezwa mwaka 2011 ukiwa unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya
Afrika.
Mkuki amesema katika
wilaya zote Mradi umeweza kukarabati barabara ili kurahisisha wakulima
kusafirisha alizeti ambapo barabara zilizokarabatiwa ni ya Muhanga-Mwakajenga
wilaya ya Manyoni kilometa 20, Njiapanda-Ngimu Wilayani Singida Kilometa 28 na
wilayani Iramba kilometa 1.4 ujenzi wake utaanza hivi karibuni.
Ameongeza kuwa mradi
umefanikisha ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi mazao kiasi cha tani
1000 katika kijiji cha Mtinko wilayani Singida, kijiji cha Nselembwe wilayani Manyoni
na kijiji cha Sanjaranda wilayani Manyoni.
Mkuki amesema mradi
wa MIVARF umewajengea uwezo wazalishaji wa alizeti kuyafikia masoko na kuongeza
thamani ya zao hilo huku akiwasisitiza wakulima kuendeleza elimu na vikundi
vilivyozalishwa na mradi huo endapo mradi utafikia ukomo wa utekelezaji wake.
No comments:
Post a Comment