Sunday, March 26, 2017

DKT. NCHIMBI AWAAGIZA WATENDAJI KUSIMAMIA MIRADI YA MAJI MKOANI SINGIDA, AAHIDI KUWASHUGHULIKIA WASIOSIMAMIA.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akijitwisha ndoo ya maji baada ya kuzindua mradi wa maji wa kijiji cha Iguguno wilaya ya Mkalama ikiwa ni maadhimishi ya kilele cha wiki ya maji yaliyofanyika katika kijiji hicho cha Iguguno, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya Mkalama Injinia Jakson Masaka.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Iguguno wilaya ya Mkalama Bi Joyce ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewaagiza watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi Mkoa kusimamia na kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya miradi yote inayotekelezwa na serikali pamoja na wahisani hasa miundombinu ya maji ambayo imekosa usimamizi wa kutosha.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji mara baada ya kusimamia makabidhiano ya mradi wa maji ulioibuliwa na halmashauri ya Iramba kabla ya kuundwa kwa halmashauri ya Mkalama ulipo mradi wa maji wa Iguguno wenye thamani ya shilingi milioni 847,099,550 na unahudumia watu elfu kumi.

Amesisitiza kuwa serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakitumia fedha nyingi kutengeneza miradi ya maji ili kuwapunguzia wananchi adha ya upatikanaji wa maji safi na salama ambapo miradi hiyo imekuwa haileti mafanikio yaliyotarajiwa kutokana na kukoa usimamizi wa kutosha.

 “Naelekeza taarifa ya miradi yote ya maji iletwe ofisini kwangu, nataka nifahamu  miradi ambayo imefikia lengo la kuwapatia wananachi maji na ile ambayo wananchi hawajaanza kunufaika kwa kupata maji safi na salama lakini fedha za umma zimetumika”, amesema Dokta Nchimbi. 

Aidha, Dkt. Nchimbi amewaaigiza watendaji wa vijiji na kata kusimamia na kutunza miundo mbinu mbalimbali ikiwemo ya maji katika maeneo yao huku akielekeza kuwa endapo uharibifu utatokea mtendaji aliyepo katika eneo husika atawajibishwa kwa uzembe. 

Awali Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Nchimbi ametembelea chanzo cha maji cha Mwankoko kinachotoa maji katika halmashauri ya manispaa ya Singida na kisha kupanda miti ili kutunza mazingira na kuhifadhi chanzo hizo.

Akitoa taarifa ya chanzo hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (SUWASA) mjini Singida Hosea Maghimbi amesema zaidi ya shilingi bilioni 1.5 sawa na asilimia 99.2  kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/17 kwa ajili ya fidia kwa wakazi walio jirani na chanzo hicho. 

Maghimbi amesema SUWASA iko katika ujenzi wa mradi wa mtandao wa maji na mfumo wa maji safi Singida mjini pamoja na kuboresha huduma ya maji  kwa miji  midogo  ya Manyoni na  Kiomboi.

Amesema baadhi ya changamoto zinazokabili  SUWASA ni  pamoja na wateja  kutolipa madeni kwa wakati hasa taasisi za serikali, wateja wanaokatiwa huduma  kwa sababu ya madeni  kutorejeshewa  huduma  hizo na badala yake  kununua maji   kwa majirani, kujifungia maji na kuchepusha dira za maji.

Maghimbi ametoa wito kwa wananchi kutokata miti, kuchoma moto, kuchungia mifungo na kufanya shughuli zangine za binadamu kwenye vyanzo vya maji.   
 
“Nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi kufichua watu wanaojiunganishia maji kiholela,   wanaojifungia maji na kuchepusha dira ya maji, kwamba SUWASA inatoa zawadi ya shillingi 50,000 kwa ye yote atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na watu hao, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria”, amesema Maghimbi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akihutubia baadhi ya wananchi wa kijiji cha Iguguno Wilaya ya Mkalama kwenye maadhimishio ya kilele cha wiki ya maji. Pamoja na mambo mengine Dkt. Nchimbi ameagiza askari wa usalama barabarani kupanda miti ya matunda ili waweze kula matunda kuboresha afya za macho yao waweze kuona vizuri kipindi wanatekeleza majukumu yao barabarani.

1 comment:

  1. Ili kuboresha usimamizi wa miundombinu ya maji vijiji na vitongoji vijiwekee sheria ndogo zitakazowasaidia kusimamia kwa ufanisi.
    Elimu ya utunzaji wa miundombinu kwa jamii itolewa

    ReplyDelete