Saturday, April 05, 2014

KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA (RCC) APRIL 5, 2014.

“Tunaweza kuongeza wingi na ubora wa mazao mara dufu bila kuongeza ukubwa wa shamba, kama wakulima wetu watafuata kwa dhati masharti na kanuni za kilimo bora, Aidha Viongozi na Wataalam  waendelee kutoa huduma zinazotakiwa ili shughuli za uzalishaji mali zilete tija kwa wananchi wa Mkoa wa Singida”, Dkt. Kone.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Parseko V. Kone akifungua kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC).
 
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone katika kikao cha ushauri cha Mkoa wa Singida wakati wajumbe wakijadili utekelezaji wa malengo ya kilimo na hali ya chakula Mkoani hadi mwezi februari, 2014.

Dkt. Kone amesema Mkoa wa Singida unajitosheleza kwa chakula kutokana na mvua zilizonyesha vizuri na uhamasishaji uliofanyika  kwa wakulima hasa katika mazao ya kipaumbele ya Uwele, Mtama, Viazi vitamu na Muhogo kwa upande wa chakula na Alizeti, Vitunguu, Pamba na Asali kama mazao ya biashara tangu mwaka 2006.
Wakuu wa Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida wakifuatilia Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Queen Mlozi, anayefuata ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba Yahya Nawanda, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Manju Msambya, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Fatma Toufiq, na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Edward Ole Lenga.

Aidha Dkt. Kone  amesema suala la ujasiriamali linapaswa kuwekewa mkazo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutenga fedha za kuwakopesha  wanawake na vijana kupitia vikundi vyao.
Ameongeza kuwa mamlaka hizo zinapaswa kutenga maeneo ya kufanyia shughuli  kwa vikundi hivyo na kuwezesha miradi midogo na ya kati  kama vile miradi  midogo midogo ya umwagiliaji, ufugaji wa kuku wa asili kibiashara na ufugaji nyuki. 
Wajumbe mbalimbali wakifuatilia Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Wa kwanza ni Mbunge viti Maalum (Chadema) Christowaja Mtinda, anayefuata ni Mbunge Iramba Mashariki Salome Mwambu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Iddi Mpanda. 
Akisoma taarifa ya maendeleo ya elimu Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Singida Fatma Kilimia amesema matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2013 Mkoa umepata ufaulu wa asilimia 56 ikiwa ni asilimia 4 zaidi ya malengo ya Matokeo Makubwa na Bayana.
 
Kilimia ameongeza kuwa licha ya ufaulu huo Mkoa umefanya ufutiliaji na kubaini kuwa bado baadhi ya walimu hawajitumi kabisa katika suala la ufundishaji, wengine hawana ujuzi wa baadhi ya mada, jamii kutokua na mwamko wa elimu hivyo kusababisha utoro na baadhi ya walimu kuandaa masomo kwa mtindo wa kizamani.

Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hizo mafunzo ya Wawezeshaji ili kuwajengea uwezo yametolewa kwa Wawezeshaji 232 kwa Halmashauri zote. 
Naye Dkt Kone ameagiza kuwa wanafunzi wote waliofaulu waweze kwenda shule na wazazi watakaokaidi wachukuliwe hatua za kisheria.


Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Singida Fatma Kilimia akisoma taarifa ya maendeleo ya elimu Mkoa wa Singida.

1 comment:

  1. Hongera Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kutuhabarisha maendeleo ya mkoa wetu, tuko pamoja katika kuleta maendeleo pongezi kwa Mkuu wa Mkoa DK Kone.

    ReplyDelete