Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameendelea na ziara yake ya kikazi kwa kukagua maendeleo ya sekta ya elimu katika Kata ya Msange, Wilaya ya Singida, ambapo ametembelea Shule ya Sekondari Msange na kutoa maelekezo mahsusi ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dendego aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa juhudi zinazofanyika katika kuinua kiwango cha elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi na ubora katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa, mabweni na vyoo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.
Aidha, alisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa halmashauri, wazazi na jamii katika kusimamia miradi ya elimu, akihimiza matumizi ya rasilimali zinazopatikana ndani ya jamii ili kuharakisha maendeleo ya shule.
Mhe. Dendego aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, Mkurugenzi wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na maafisa kutoka Ofisi ya Elimu Mkoa na Wilaya, katika kuhakikisha hatua za kimaendeleo zinatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuendelea kushirikiana bega kwa bega na wilaya hiyo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Aliahidi kusimamia kwa ukamilifu maagizo yote yaliyotolewa ili kuwaletea wananchi maendeleo yanayoonekana.
Ziara hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Mkoa wa Singida wa kufuatilia na kuhimiza maendeleo katika sekta ya elimu, sambamba na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kutoa elimu bora, jumuishi na yenye usawa kwa watoto wote wa Kitanzania.
No comments:
Post a Comment