Friday, April 11, 2025

RC DENDEGO AWAPONGEZA REA KUFIKISHA UMEME VIJIJINI

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amepongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi kubwa ya kufikisha umeme vijijini hali iliyobadili maisha ya wananchi vijijini.

Mhe. Dendego ametoa pongezi hizo Aprili 11, mkoani Singida wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Mwaka kati ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG) pamoja na REA uliolenga kupitia bajeti na mpango kazi wa Wakala huo kwa mwaka 2025/26.


“Nishati ya umeme ni nguzo kubwa kwa maendeleo ya Taifa lolote na watu wake. Nishati ya umeme vijijini ni msingi mkuu wa kuimarisha maendeleo ya haraka katika vijijini vyetu. Sote tumeshuhudia matokeo makubwa kwenye ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha ya jamii zetu pamoja na kuchagiza utoaji wa huduma za kijamii".

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatib Kazungu amewashukuru Wabia hao wa Maendeleo na kusema kuwa wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini huku akiwahakikishikia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha lengo la kuwafikishia nishati bora kwa bei nafuu wananchi wote linafikiwa.


Awali akizungumza, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meje Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amesema kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na mafanikio hayo yametokana na dhamira ya Serikali pamoja na mchango wa Wabia wa Maendeleo na kuahidi kuwa, REB itaendelea kuisimamia Mejimenti ya REA kuhakikisha miradi yote iliyopangwa inafanikiwa kwa wakati na katika ubora uliokusudiwa.











         *KARIBU SINGIDA:MEI MOSI 2025*

No comments:

Post a Comment