Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amefungua rasmi Mkutano wa Wakuu wa Shule za Sekondari wa Kanda ya Kati unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Chuo cha Uhasibu (TIA), Singida, kuanzia tarehe 10 hadi 11 Aprili 2025, akitoa rai kwa walimu na viongozi wa shule kuhakikisha elimu inaimarishwa kwa misingi ya maadili, uzalendo na uwajibikaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo unaowakutanisha wakuu wa shule kutoka mikoa ya Singida na Dodoma, Mhe. Dendego ameeleza kuwa ni wakati wa kuwekeza nguvu kubwa katika kupambana na changamoto sugu zinazoikabili sekta ya elimu, hasa utoro wa wanafunzi, mimba za utotoni, na kushuka kwa maadili mashuleni.
“Lazima tushirikiane kuhakikisha tunalinda maadili ya vijana wetu. Wanafunzi wakilelewa vizuri shuleni, taifa linajenga msingi imara wa viongozi wa baadaye,” amesema.
Ameeleza kuwa mikutano ya aina hii ya kitaaluma ni muhimu kwa kuwa inatoa nafasi kwa wakuu wa shule kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto kwa pamoja na kutoa suluhisho zinazotekelezeka kwa lengo la kuinua ubora wa elimu nchini.
Aidha, aliupongeza umoja wa wakuu wa shule kupitia TAHOSA kwa kuendelea kushikamana, kusimamia maendeleo ya taaluma pamoja na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya serikali, hususan ile ya miundombinu ya elimu inayotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nyie wakuu wa shule mmekuwa viongozi mstari wa mbele katika utekelezaji wa miradi ya elimu – mmekuwa wahandisi wa maendeleo. Hongereni sana kwa uzalendo na uaminifu,” alisema Dendego kwa msisitizo.
Pia,RC Dendego ametumia jukwaa hilo pia kuwakumbusha walimu kushiriki kikamilifu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo mwaka huu yanafanyika kitaifa mkoani Singida, akisema hiyo ni fursa ya kipekee kwa walimu kuonesha mshikamano wao kama sehemu ya watumishi wa umma.
Kwa upande wao, viongozi wa TAHOSA walisema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuimarisha uratibu wa shughuli za kitaaluma na kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa serikalini kuhusu maboresho ya sekta ya elimu.
Mkutano huu wa siku mbili unaendelea kujadili mada mbalimbali zikiwemo za uongozi wa shule, malezi ya wanafunzi, usimamizi wa mitihani, matumizi ya TEHAMA katika kufundishia, na kuboresha mazingira ya kufundishia kwa kutumia rasilimali zilizopo.
No comments:
Post a Comment