Zoezi hilo limezinduliwa kupitia kikao kazi cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, kikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Halima Dendego kikijumuisha wataalamu wa afya, viongozi wa kisiasa na kidini, pamoja na maofisa kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo walioeleza kwa kina umuhimu wa kampeni hiyo ya kitaifa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewataka viongozi wa dini na kisiasa kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa chanjo hiyo ili kufanikisha kampeni hiyo na kulinda afya ya watoto. Aidha, aliiomba Wizara ya Afya kutumia maabara za ndani ya nchi badala ya kutuma sampuli nje, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza gharama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mhe. Maltha Mlata, amesema ni muhimu kuwapa wazazi na watoto elimu ya kutosha kabla ya kupewa chanjo ili kupunguza hofu. Pia amewahimiza viongozi wa afya kushirikiana na waganga wa jadi ambao mara nyingine huathiri mitazamo ya wananchi kuhusu chanjo.
Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Mwezeshaji wa Kitaifa wa Chanjo ya Polio kutoka Wizara ya Afya, Bw. Bakari Hamad Bakari, amesema kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa dozi ya pili ya sindano ni kuongeza kinga ya mwili dhidi ya virusi vya polio ambavyo bado ni tishio kwa watoto nchini Tanzania, hasa kutokana na mwingiliano wa watu kutoka mataifa yenye maambukizi. Alisema virusi vya polio vinaweza kuingia mwilini kupitia maji au chakula kilichochafuliwa, hukaa kwenye utumbo, kuongezeka kwa kasi na baadaye kuvamia mfumo wa fahamu na kusababisha kupooza.
Bw. Bakari ameeleza kuwa licha ya kuwa na chanjo ya awali ya matone, dozi ya pili ya sindano imeongezwa ili kuhakikisha watoto wanapata kinga ya kutosha, kwani watoto walio chini ya miaka mitano ndio waathirika wakuu wa polio. Amesisitiza kuwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa, kichwa kuuma, kutapika na kuhara, lakini mara nyingi mgonjwa hugundulika wakati tayari ameanza kupata ulemavu wa kupooza. Alionya kuwa mtoto yeyote chini ya miaka 15 anayepata kupooza ghafla bila sababu za ajali au kuumia ubongo, anapaswa kuchunguzwa kwa haraka kama mshukiwa wa polio.
Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe waliibua maswali kuhusu usalama wa chanjo na wito wa kuhakikisha elimu kuhusu huduma hiyo inaendelea kutolewa mara kwa mara ili kuondoa hofu miongoni mwa wazazi ambapo Mratibu wa Huduma ya Chanjo Mkoa wa Singida, Bw. Habib Mwinory, aliwahakikishia wajumbe kuwa chanjo itatolewa katika vituo vya afya kwa utaratibu wa kawaida, bila kufanya kampeni mashuleni. Aliongeza kuwa watoto watakaopata madhara madogo baada ya chanjo watahudumiwa ipasavyo na wahudumu wa afya.
Bw. Bakari alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa haraka kwa vituo vya afya endapo mtoto atapata dalili zozote za kushukiwa kuwa na polio, ili hatua zichukuliwe mapema. Alisisitiza pia umuhimu wa matumizi ya maji safi na salama, pamoja na kujenga utamaduni wa kupima afya badala ya kusubiri hali kuwa mbaya. Alisema kupima afya mapema ni hatua muhimu ya kuzuia madhara ya magonjwa sugu kama polio.
Kampeni ya utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ya polio kwa njia ya sindano ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya polio, ikiwa ni hatua ya kuimarisha afya ya watoto na vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment