Friday, April 04, 2025

KUKU FESTIVAL MEI MOSI SINGIDA MAANDALIZI YAMEKAMILIKA

.        Mkuu  wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, amewataka wafanyabiashara wanaochoma nyama ya kuku mjini Singida kujipanga kwa ajili ya kutoa huduma hiyo vizuri kwa mamia ya wageni ambao watakuja  kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) ambayo yatafanyika kitaifa mkoani hapa.

Alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza saa 3:00 usiku akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mheshimiwa Godwin Gondwe, Meya wa Manispaa ya Singida Mhe.Yagi Kiaratu, Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Bi.Naima Chondo katika eneo la Ubungo Singida mjini ambalo ni maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wanaofanya biashara ya kuchoma nyama ya kuku kwa saa 24.

"Tumekuja kuwatembelea hapa kuona hali ilivyo hapa ili wageni wetu watakaokuja kwa ajili ya Mei Mosi wasijisikie vibaya, tunategemea zaidi ya wageni 6000 katika mjini wetu wa Singida na wote wataishi hapa Manispaa ya huduma zote wanategemea kuzipata hapa hapa,"alisema.

Mhe.Dendego amesema kutokana na ugeni huo mkubwa kila mfanyabiashara ajipange kwa kuhakikisha anatoa huduma nzuri na katika mazingira safi ili hata watakapokuwa wameondoka wasimulia jinsi kuku wa Singida walivyo wazuri na watamu.

Naye Meya wa Manispaa wa Singida, Yagi Kiaratu, alishukru kwa mkoa wa Singida kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa siku ya Mei Mosi kwani hali hii itaweza kuongeza kipato kwa wananchi wa Manispaa ya Singida ambao watatumia fursa hiyo kufanya biashara mbalimbali.

"Singida ni mkoa ambao vyakula vya asili vinapatikana, hapa wageni wetu wakija watakula kuku wa asili, ng'ombe wa asili wageni watafurahia vyakula vizuri na vitamu na sisi tumejipanga kutoa huduma kwa kukesha hadi asubuhi," alisema.

Naye Katibu wa Wafanyabiashara Wachoma Kuku eneo la Ubungo, Joseph Raphael, aliishukru serikali kwa kuileta Mei Mosi kitaifa Singida na kwamba wamejipanga kutoa huduma nzuri za nyama ya kuku.

Alisema changamoto zilizopo katika eneo hilo watahakikisha wanazimaliza ili wageni wakija waweze kupata huduma nzuri za chakula na kwamba kwa sasa wameanza kutumia nishati safi ya gesi ili kuweza kuwahudumia kwa uharaka zaidi.

Kabla ya kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi shughuli mbalimbali zitafanyika kama vile michezo,utalii wa barabarani lengo likiwa kuwaonyesha wageni wataofika Singida wajue Singida kuna utalii gani.

Sambamba na maandalizi hayo,Mei Mosi Mkoani Singida linatarajiwa kuwa na usiku wa Kuku ( kuku festival), mashindano ya magari, ngoma za asili, makongamano na bonanza la michezo litakaloanza wiki mbili kabla ya kilele cha Mei Mosi


                 *KARIBU SINGIDA-MEI MOSI 2025*

                         S I N G I D A      N I   S A L A M A

No comments:

Post a Comment