Singida, Aprili 12, 2025
Serikali ya Mkoa wa Singida imetangaza msimamo mpya kuhusu udhibiti wa ongezeko la watoto wa mtaani, ikisisitiza ushirikiano wa familia, viongozi wa dini, jamii na taasisi za serikali katika kuimarisha malezi na kusaidia watoto waliotengwa kurejea kwenye mazingira salama.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Mtaani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social jijini Singida, Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Fatuma Mganga, alisema kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa familia au huduma muhimu kwa sababu ya migogoro ya kifamilia, mmomonyoko wa maadili, au uzazi usio na uwajibikaji.
"Malezi bora siyo kumpendeleza mtoto tu—wakati mwingine lazima achapwe ili akue. Lakini pia watoto wajue kuwa kufundishwa na kusahihishwa si mateso. Mitaani hakuna mzazi, hakuna usalama, na hakuna upendo wa kweli," alieleza Dkt. Mganga.
Alisisitiza kuwa wanaume wanapaswa kuwajibika katika malezi na kuacha tabia ya kukwepa majukumu baada ya mimba, jambo linalosababisha ongezeko la watoto wa mtaani.
"Hali ya maambukizi ya VVU kwa wasichana wadogo ni ya kutisha, na chanzo kikubwa ni wanaume wazima kuwarubuni watoto wa kike. Tukatae tamaa hizi na tuwalinde watoto wetu wote—wa kike na wa kiume," alisema Dkt. Mganga.
Afisa Ustawi wa Mkoa wa Singida, Bw. Edward Maselo, alisema kuwa takribani watoto 150 waliathirika kutokana na migogoro ya kifamilia, hasa kuvunjika kwa ndoa, jambo lililosababisha baadhi yao kukimbia familia na kuishi mitaani.
“Tumeendelea kuwafuatilia watoto hawa na kuwapatia huduma muhimu kama chakula, mavazi, elimu, na afya. Pia tunawaelimisha wazazi kuhusu malezi bora, huku tukitayarisha kampeni maalum za kuelimisha jamii juu ya haki za mtoto,” alieleza Bw. Maselo.
Afisa Ustawi wa Manispaa ya Singida, Bi. Dorah Simon, alifafanua kuwa maadhimisho hayo yamelenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu changamoto zinazowakumba watoto wa mtaani na umuhimu wa jamii kuwatambua kama sehemu ya familia kubwa ya taifa.
“Watoto hawa wana haki ya elimu, afya, ulinzi na malezi kama watoto wengine. Jamii iwakumbatie na iwasaidie kurudi kwenye maisha ya kawaida,” alisema Bi. Dorah.
Katika tukio hilo, watoto waliowahi kuishi mitaani walitoa ushuhuda kuhusu maisha yao kabla na baada ya kupatiwa huduma na msaada wa kijamii. Pia, viongozi wa dini walihamasishwa kushiriki kikamilifu katika kuwaelekeza watoto katika maadili mema, hususan watoto wa kiume ambao wameripotiwa kuwa wachache katika nyumba za ibada.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa na kuhitimishwa kwa wito wa ushirikiano kutoka kwa wadau wote wa jamii kuhakikisha watoto wa mtaani wanapewa fursa ya pili ya maisha bora.
No comments:
Post a Comment