Thursday, June 27, 2024

WATAKAOTUKANA VIONGOZI WAKUU WA SERIKALI MKOANI SINGIDA KUKIONA CHA MOTO - RC SINGIDA

Serikali ya mkoa wa Singida imeonya wanasiasa au mtu yeyote atakayeingia mkoani humo na kuanza kukashifu na kutukana Viongozi wa Juu wa Serikali atakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

Mkuu wa mkoani Singida Halima Dendego, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ametoa kauli hiyo (27/Juni/2024) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Stendi ya Itigi kwa ajili kusikiliza na kero zinazowakabili wananchi wa Halmashauri ya Itigi na kuzitafutia majawabu.

Rc Dendego amesisitiza kuwa hatakubali Viongozi Wakuu wa Serikali watukanwe na kudhalilishwa mkoani humo wakati yeye yupo hivyo ameonya kuwa watakaothubutu kufanya hivyo watakiona cha moto.

Amesema kuwa wananchi wa mkoa wa Singida ni watu wa amani na wanataka maendeleo ikiwemo barabara maji shule afya mbolea na sio mambo ya matusi hivyo kwa yeyote anayetaka kuvunja amani na utulivu kwa maslahi yake binafsi watashughulika nae.

“Vijana wa mkoa wa Singida achene kukaa kimya Viongozi wanapotukwana bali muwajibu kikamilifu kupitia mitandao ya kijamii kuhusu kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, Ameeleza Dendego.

Amewataka wananchi wa mkoa wa Singida kwa umoja wao kuwakataa baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuwagawa wananchi kwa udini, ukabila au rangi kwa sababu Watanzania wote ni wammoja tangu enzi na wanashirikiana katika masuala mbalimbali ya kijamii.

Rc Dendego pia ameeleza kuwa Vyama vya siasa vilianzishwa nchini ili vishindane kwa hoja na sio matusi kwenye majukwaa na kusema ukiona baadhi ya vyama vinafanya hivyo basi havina sera na hakuna sababu ya wananchi wa mkoa huo kwenda kwenye mikutano yao.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Singida Martha Malata, akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi katika Halmashauri ya Itigi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Singida Martha Malata, amewataka wananchi wa mkoa wa Singida kuwapuuza baadhi ya wanasiasa wanakuja mkoani humo kufanya siasa za uhasama na uchochezi.  

Mlata amewahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Sita kwa sababu imeonyesha dhamira ya dhati katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu katika sekta zote ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, (wapili kutoka kushoto) akimsikiliza moja wa mwananchi wa Halmashauri ya Itigi mara baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Martha Mlata, kuzungumza kwenye mtutano huo.  


No comments:

Post a Comment