Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, ameagiza kuchukuliwa hatua kwa Wakuu wa Idara ambao watazalisha hoja mpya za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama hatua ya kuimarisha utendaji kazi kwenye Halmashauri hizo.
Mkuu huyo wa
Mkoa wa Singida ametoa kauli hiyo (26/Juni/2024)
katika Kikao Maalum cha kujadili hoja za CAG cha Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Dendego
ametoa agizo hilo kufutia Halmashauri ya Manispaa ya Singida kuwa na hoja 64
kutoka mwaka wa fedha 2011 hadi Juni 2024 ambazo hazijafungwa jambo ambalo
amesema sio zuri na linatia dosari katika kutekeleza sheria, kanuni na taratibu
za Serikali hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameonya kuwa
hataki kusikia uzalishaji wa hoja mpya zinazalishwa tena na kama zikitokea basi
aliyesababisha hoja hiyo aitwe na kuhojiwa kwa nini hoja hiyo imetokea
ikiwezekana achukuliwe hatua kwa kusababisha hoja hiyo.
Amesema hoja
hizo zinapotokea zinasababishwa na kuwepo kwa kasoro hasa katika usimamizi hafifu
wa miradi ya maendeleo.
Naye, Katibu
Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga ameonyesha kukerwa na uwajibikaji
hafifu wa Watendaji wa Manispaa ya Singida katika kujibu hoja za CAG licha ya
ushauri uliowapatia katika kikao cha Kamati ya Fedha.
Dkt. Mganga
amesema mambo mengi walioshauri ambayo yangesaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza
hoja za CAG hayajafanyiwa kazi jambo ambalo ameonya lazima likome na Watendaji
lazima wawajibike ipasavyo katika kuondoa kasoro hizo.
Amewataka
Wakuu wa Idara katika Halmashauri za mkoa huo kuacha uzembe na kuhakikisha
hawazalishi hoja mpya za CAG na kujibu kwa uhakika hoja zilizopo ili ziweze
kufungwa na CAG.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu, amemhakikishia Mkuu wa mkoa wa Singida kuwa watafanyia kazi maelekezo yao ili kuhakikisha hoja 64 za CAG zinafanyiwa kazi ili kuhakikisha Manispaa ya Singida inakuwa bora katika utendaji wake wa kazi.
Mkaguzi Mkuu Ofisi ya Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Singida Othman Jumbe, akishauri jambo kwenye mkutano huo maalum wa baraza la Madiwani kujadili hoja za ukaguzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Mkutano ukiendelea
Wakuu wa Idara na Vitengo wa Manispaa
ya Singida wakiwa kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za CAG.
Sehemu ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida wakishiriki mkutano huo maalum wa baraza la Madiwani kujadili hoja za ukaguzi Singida mjini.
No comments:
Post a Comment