
Mkuu wa Mkoa
wa Singida Halima Dendego, ameonya kuwa hatapenda kusikia miradi yoyote ya
maendeleo inayoibuliwa katika Halmashauri za mkoa huo inakwama kwa kisingizio
cha kutaka kuongezewa fedha za ziada.
Mkuu huyo wa
mkoa wa Singida ametoa kauli hiyo (28 Juni, 2024) katika Kikao Maalum cha
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mkalama cha kujadili hoja za Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Amesema kuwa
kuanzia sasa Halmashauri zote zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha miradi
iliyopo kwanza ikiwemo maboma yote yaliyojengwa kabla ya kuanzisha miradi mipya.
Aidha, Rc
Dendego pia amewaagiza Madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo badala ya wao nao kuanza kulalamika kuwa
miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao haikamiliki.
“Madiwani mnatakiwa kusimamia
kikamilifu miradi ya maendeleo kwenye maeneo yenu na miradi hiyo ilete matokeo
chanya kulingana na thamani ya fedha”, Amesisitiza Dendego.
Naye,Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga,
amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani humo kuwa wabunifu katika utekelezaji
wa miradi ya maendeleo ikiwemo kuajiri kwa mkataba Wahandisi waliostaafu na
mafundi wenye ujuzi wa kujenga ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo ya wananchi.
Dkt. Mganga amesema anajua uhaba wa Watumishi hasa kwenye
kada ya Uhandisi lakini isiwe ndio kisingizio cha miradi kukwama hivyo ni
muhimu Wakurugenzi wakawa na njia mbadala ya kuhakikisha miradi ya maendeleo
inatekelezwa kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa.
Amesisitiza kuwa miradi yote ya maendeleo ambayo bado haijakamika lazima iingizwe kwenye bajeti mpya ili ujenzi wake uweze kukamilika.
Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akitoa maelekezo ya Serikali kwa Watendaji wa Halmashauri ya Mkalama kuhusu namna ya kupunguza hoja za CAG pamoja na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkalama James
Mkwega, amemshuruku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan, kwa kuipatia fedha nyingi Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.
Mkwega amesema tangu aanze kazi ya udiwani hajawahi kuona
fedha nyingi zinazotolewa na Serikali kama kipindi hiki hivyo wao kama Madiwani
wanajukumu kubwa la kuhakikisha miradi inayoteelezwa kwenye maeneo yao inakuwa
bora kulingana na thamani ya fedha.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Mkalama James Mkwega akizungumza wakati akifungua Kikao cha
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mkalama kwa ajili ya kujadili hoja za CAG.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mosses Machali, akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mkalama kwa ajili ya kujadili hoja za CAG.
Mkaguzi Mkuu Ofisi ya Mdhibiti wa Hesabu za Serikali mkoa wa Singida Othman Jumbe, akitoa ushauri kwa watendaji wa Serikali kwenye kikao hicho.
No comments:
Post a Comment