Saturday, June 29, 2024

RC DENDEGO - VIKUNDI VYA WANUFAIKA WA MIKOPO YA HALMASHAURI MKOANI SINGIDA VYATAKIWA KUREJESHA

Serikali ya mkoa wa Singida imewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Polisi wa Wilaya mkoani humo kuwasaka na kuwakamata watu wote (vikundi) waliochukua mikopo ya asilimia 10 kwenye Halmashauri mkoani Singida ili warejeshe kulingana na kiasi kilichokubaliwa katika mkataba wa mkopo.

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego, ametoa kauli hiyo katika kikao cha Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Iramba cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Rc Dendego ametoa mfano kwa Halmashauri ya Iramba pekee zaidi ya Milioni 118 hazijarejeshwa mpaka sasa na kusisitiza kuwa tatizo lazima litafutia ufumbuzi kwa wahusika kukamatwa ili warejeshe mikopo hiyo.

“Nataka Dc na OCD muwasake popote walipo watu waliokopeshwa fedha hizo ili wazirejeshe ili wananchi wengine wakopeshwe,” Amesisitiza Dendego.

Aidha, RC Dendego amesisitiza kuwa vikundi vyote vya wanufaika wa mikopo hiyo kuanza marejesho haraka iwezekanavyo na wote watakaokaidi agizo hilo wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa muujibu wa kisheria taratibu na kanuni za mkataba.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoani humo washirikiane na Viongozi wengine katika kusaka Vikundi vilivyokopeshwa fedha hizo na kuzirejesha haraka vinginevyo nao watawajibishwa mpaka hapo vikundi hivyo vilipe fedha hizo kwa sababu wao wanavijua.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi, ameunga mkono hoja ya wanachama wa vikundi vilivyokopeshwa fedha za Halmashauri kusakwa ili warejeshe fedha hizo.

Msengi amesema fedha hizo zinazodaiwa ni nyingi hivyo lazima nguvu ya ziada itumike ili kuhakikisha waliokopeshwa wanazirejesha ili wananchi wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo ya Halmashauri.

Mwenyekiti huyo pia amemshukuru Rais Samia kwa kuipatia Halmashauri hiyo zaidi ya shilingi Bilioni Tatu kwa ajili ya kutelekeza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika sekta za afya na elimu.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akizungumza kwenye kikao hicho.


Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba CPA Joseph Komanya, akisoma hoja za CAG kwenye kikao hicho.



Mkaguzi Mkuu Ofisi ya Mdhibiti wa Hesabu za Serikali mkoa wa Singida Othman Jumbe akizungumza kwenye kikao hicho. 


No comments:

Post a Comment