Tuesday, September 05, 2023

RC SERUKAMBA: SINGIDA INAWEZA KUWA KINARA UKUSANYAJI MAPATO KILA MTU AKIWAJIBIKA

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema Mkoa huo unaweza kuwa kinara wa ukusanyaji wa mapato, uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa miradi iwapo tu watendaji watafanya kazi kwa kujituma na kushirikiana badala ya kuyaachia baadhi ya makundi kufanya kazi hiyo.

Serukamba amesema hayo jana ( 4 Septemba, 2023)  wakati akizungumza na Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri na wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri za Mkoa wa Singida katika kikao kazi kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida.

Alisema  Halmashauri zinatakiwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha mashine za kukusanya fedha (POSS) zisitumike feki.

Alisema kumekuwa na changamoto ya ukusanyaji wa mapato na matumizi ya POSS feki hivyo kuukosesha mkoa kupata mapato stahiki ambapo aliviomba vyombo vya dola ikiwamo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kusaidia kufanya uchunguzi kwenye mageti ya ukaguzi wa mazao yanayosafirishwa.

'' Tukifanya kazi vizuri katika uhifadhi wa mazingira, ukusanyaji mapato, ukamilishaji wa miradi kwa wakati na kuwa timu moja, siku moja  tutakuwa namba moja kitaifa,'' alisema Serukamba.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga akizungumza kwenye kikao hicho aliwaomba Wakurugenzi pindi wanapopokea fedha za miradi kabla ya kuanza kutekelezwa watoke ofisini na kwenda kujua bei za vifaa badala ya kuwaachia watu wa manunuzi pekee ambao wamekuwa na changamoto ya kuweka bei ya juu.

'' Miradi mingi imekuwa haikamiliki kutokana na fedha zilizotolewa na Serikali kumalizika kabla haijaisha na hiyo inasabishwa kununua vifaa kwa bei kubwa lakini Wakurugenzi wakitoka na timu yao watawakuta wauzaji wa vifaa hivyo kwa bei ya chini.'' alisema Dkt. Fatuma Mganga.

Mganga akitolea mfano alisema alipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri wakati wanataka kutegeneza milango waliwaomba watu wa manunuzi wawape bei yao ambapo walisema ni Sh.Milioni 72 na walipotoka kutafuta bei kwa watu wengine alikuwepo wa Sh.Milioni 50 na mwingine Sh.Milioni 48 na hivyo kumpa kazi hiyo aliyekuwa na bei ya chini ambaye alifanya kazi hiyo kwa viwango vya hali ya juu.

Katika hatua nyingine Mganga aliwaomba Wakurugenzi hao kujenga tabia ya kwenda kujifunza kwa wenzao ambao wanafanikiwa kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati na kwa fedha zilezile walizopokea kama wao.

Alisema utakuta Serikali imetoa fedha kiwango sawa lakini katika ukamilishaji wa miradi kwa fedha hizo hizo Halmashauri zingine zinakamilisha miradi iwe ya ujenzi wa shule au kituo cha afya na halmashauri nyingine utakuta ujenzi wake upo hatua ya msingi.

Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya walitoa taarifa za ukusanyaji wa mapato pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye Wilaya zao.

No comments:

Post a Comment