Saturday, September 30, 2023

MKOA WA SINGIDA WAKABIDHI MWENGE WA UHURU KWA KISHINDO. *JUMLA YA MIRADI 42 YENYE THAMANI YA TSH. BILIONI 15.3 IMEKUBALIWA*

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba jana tarehe 29 Septemba, 2023 amekabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Ally Gugu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Rosemary Senyamule huku jumla ya miradi ya maendeleo ikiwa ni 42 yenye dhamani ya Tsh Bilioni 15.3 iliyokuwa inapitiwa na Mwenge wa Uhuru imekubaliwa.

Mwenge wa Uhuru ulipokelewa Mkoani Singida tarehe 22 Septemba, 2023 kutoka Mkoani Tabora na kukimbizwa kwa muda wa siku 7 katika Wilaya 5 zenye Halmashauri 7 kwa kuanzia Iramba na kuhitimisha Wilayani Manyoni kwa lengo la kufikisha ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2023 ukikagua miradi ya ujenzi nyaraka za manunuzi kuweka jiwe la msingi kufanya uzinduzi ambapo imeelezwa miradi yote imetekelezwa kwa viwango.

Aidha Wananchi wa Mkoa wa Singida wamepokea vema ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 ambao umetolewa maeneo mbalimbali ya Halmashauri za Mkoa huo ambao ni “Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa”.

Hata hivyo Dkt. Fatuma Mganga amemshukuru na kumpongeza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim pamoja na wenzake wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa kuleta ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu kwa umahiri mkubwa.

“Wananchi wa Mkoa wa Singida kwa pamoja kupitia ujumbe huo mwambatano wa Mwenge wa Uhuru tumejifunza kuhusu : -

Mapambano dhidi ya Rushwa, chini ya Kauli mbiu “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu: Tutimize Wajibu Wetu”.

Mapambano dhidi ya Malaria, chini ya kauli mbiu “Ziro Malaria Inaanza na Mimi – Nachukuahatua kuitokomeza”.

Mapambano dhidi ya Dawa za kulevya, chini ya kauli mbiu “Tukabiliane na Changamoto za Dawa za Kulevya wakati Wote kwa Ustawi wa Jamii”.

Mapambano dhidi ya VVU / UKIMWI chini ya kauli mbiu “Imarisha Usawa, Tokomeza Ukatiliwa Kijinsiana Unyanyapaa”.

Lishe Bora kwa afya imara, chini ya kauli mbiu “Lishe ni Msingi wa Maendeleo Sote Tuwajibike”. Dkt. Fatuma Mganga

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim akizungumza na wananchi Wilayani Manyoni wakati wa shamrashamra za Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 Mkoani Singida.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib Kaim, ameeleza kuwa miradi yote iliyotembelewa katika Mkoa wa Singida na Halmashauri zake imeonekana kutekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na Serikali. Aidha amewasisitiza Wakurugenzi na Wakuu Wilaya kuhakikisha wanafanyia kazi ushauri na maelekezo yaliyotolewa kwa baadhi ya miradi kwa ajili ya kuboresha zaidi.

Sambamba na hilo Kaim ameelekeza kwa watendaji wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia miradi yote ya maendeleo na kuikamilisha kwa wakati ili iweze kutumika kama ilivyo kusudiwa.

Katika mbio hizo za Mwenge wa Uhuru miradi mbalimbali ilionekana kuwagusa zaidi wananchi katika Mkoa wa Singida ambapo ni utekelezaji wa miradi ya barabara, miradi ya maji, sekta ya Elimu, Sekta ya Afya pamoja na miradi mbalimbali ya vijana.

Pamoja na mambo mengine wananchi wameeleza kuwa miradi iliyozinduliwa na kuwekewa jiwe la msingi ni miradi muhimu kwa maendeleo ya wananchi na itasaidia kupunguza kero ambazo zilikuwa zikionekama kuwa sugu.

Baadhi ya wananchi wamesema miradi ambayo inahusika na sekta ya maji itasaidia kupunguza adha waliyokuwa wakiipata wakina mama kutembea umbali mrefu kufuata maji pamoja na kuwapa uhakika wa kupata maji safi na salama.

Wananchi hao kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa ujenzi wa vituo vya Afya na Zahanati pamoja na ugawaji wa vyandarua kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano itasaidia kupunguza maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria pamoja na kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto kwa kuwa huduma hiyo imewasogelea wananchi.

Hiyo kama haitoshi wameeleza kuwa uwepo wa barabara za uhakika zilizowekewa jiwe la msingi zitachochea maendeleo kwa maana zitafanya watu kutumia muda sahihi hususani kwa wafanya biashara.




"MUNGU BARIKI MBIO ZA MWENGE WA UHURU MWAKA 2023 NA WAKIMBIZA MWENGE KITAIFA.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

MWENGE WA UHURU HOYEEEE!!!!!!!!".

No comments:

Post a Comment