Mkoa wa Singida leo tarehe 1 Oktoba, 2023 umeadhimisha Siku ya Wazee Duniani kwa kuwapatia Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF) Wazee miamoja (100) wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo na kuhusisha wawakilishi kutoka Halmashauri zote saba za Mkoa huo.
Akizungumza katika
maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida katika Siku ya Wazee
Duniani Jimson Mhagama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni amesema suala la Wazee kupatiwa vitambulisho vya matibabu ni agizo la
Serikali ili kuhakikisha wanatambuliwa na kupewa huduma stahiki.
Mhagama amepongeza
hatua nzuri iliyofikiwa katika uundwaji wa mabaraza ya wazee ambapo mabaraza ya
Wazee 637 kati ya hayo mabaraza 151 sawa na asilimia 24 yamejengewa uwezo
katika Mkoa wa Singida ili kuhakikisha huduma na maslai ya Wazee yanapatikana.
“Niwapongeze sana
wadau wetu wa maendeleo kwa kazi kubwa mliofanya ya kuhakikisha wazee
wanajengewa uwezo wa Sera ya wazee ya mwaka 2003 pamoja na majukumu ya viongozi
wa mabaraza ya Wazee katika ngazi mbalimbali”
“Nawaelekeza
Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha mabaraza ya Wazee yanafanya vikao
vyao kila robo kama miongozo inavyoelekeza ili kuwezesha ufanisi katika kazi
zake”. Amesema Mhagama kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.
Aidha Serukamba ametoa
rai kwa Jamii hasa ndugu wa karibu kuacha tabia ya kuwanyang’anya Wazee maeneo
yao (ardhi, nyumba nk) jambo linalopelekea Wazee kukosa mwelekeo. Hivyo amesisitiza
kuwa kitendo hicho ni kinyume na Sheria, na wale watakaobainiki Sheria
itachukua mkondo wake.
Akizungumzia suala la
malezi ya watoto, Mhagama kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesisitiza umuhimu wa
wazazi kuwalea watoto wao ili kuwajengea stadi mbalimbali za maisha na kufanya
wawe raia bora.
Kwa upande wa wazee
wanaonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Serikali Mkoani Singida
imesajili kaya zipatazo elfu 58,760 zinazonufaika wakiwemo wazee, kati ya kaya
hizo watoto ni elfu 1,318 kutoka kaya maskini ni wanufaika wa mfuko huo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa
wa Singida Peter Serukamba kupitia kwa mwakilishi wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ametoa wito kwa vijana kuwatunza wazee wao
ambao ni hazina kwa kuwatimizia mahitaji yao mbalimbali ikiwemo chakula ili
kuepuka Wazee kuzunguka mitaani wakiombaomba.
Akimalizia hotuba yake
Mkuu wa Mkoa wa Singida iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Manyoni amewakumbusha na kuwaomba wazee kuendelea kusisitiza suala la
malezi chanya kwa watoto na maadili mema kwa vijana ili kujenga jamii isiyokuwa
na mmomonyoka wa maadili.
Mkoa wa Singida unandelea
kuboresha huduma za Afya kwa Wazee, huduma za matunzo kwa Wazee wasio kuwa na
uwezo kwa kuwatengea makazi yaliyopo Sukamahela katika Wilaya ya Manyoni Mkoani
humo.
Kauli mbiu ya mwaka
huu (2023) ambayo ni “Uthabiti wa Wazee kwenye dunia yenye Mabadiliko.
“Kauli mbiu hiyo inamaanisha kuwa Dunia inapitia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kisiasa na dhihiri kuwa Wazee wamekuwa imara kwenye kukabiliana na mabadiliko hayo”.
No comments:
Post a Comment