Askari
wa usalama barabarani mkoani Singida, E.8763. Sgt. Benes Lucas akikagua mabasi
yanayotumika kusafirisha wanafunzi mjini hapa jana.
Baadhi ya mabasi kati ya 20 yanayotumika kusafirisha wanafunzi Mkoani
Singida yakifanyiwa ugazi na askari usalama barabarani kwa lengo la
kujiridhisha ubora wake.
Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani Mkoa
wa Singida limeanzisha zoezi kambambe la kukagua mabasi yanayotumika
kusafirisha wanafunzi huku likisisitiza kuwa zoezi hilo kuwa endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya kamanda wa jeshi la polisi
Mkoa wa Singida, RTO Mrakibu wa Polisi Peter Raphael Majira, amesema
zoezi hilo lililoanza jana litaendelea kwenye wilaya zote za mkoa wa Singida.
Amesema lengo ni kuhakikisha mabasi hayo yanakidhi
mahitaji yote ya sheria za usalama barabani, wakati wote yanapokuwa
barabarani.
Amesema pia wanatoa elimu na wanawakumbusha
madereva na wamiliki wa mabasi hayo, juu ya wajibu wao na umuhimu wa kuzingatia
kwa umakini mkubwa sheria za usalama barabarani.
Aidha RTO Peter amesema wanawakumbusha
madereva kujenga utamaduni wa kuwa na tahadhari zaidi na kitendo hicho
kitapunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani.
Pia ametumia fursa hiyo kuwataka wenye watoto
wanaotumia mabasi hayo wahakikishe mtoto anakaa kwenye kiti chake na si
kuchangia kiti.
“Mzazi/mlezi usikubali kabisa mwanao achangie kiti,
umelipitia kiti kwa nini achangie na wanafunzi mwingine. Na ninyi wamiliki wa
mabasi haya kama kuna hafla wanafunzi wanakwenda kuhudhuria iwapo wamejaa
(yaani kila mwanafunzi ana kiti chake), peleka hao waliopata viti halafu urudie
wengine” amesisitiza mrakibu Peter.
Kwa upande wao madereva hao wamelipongeza jeshi la
polisi mkoa wa Singida kwa kuendesha ukaguzi huo na kuwakumbusha juu ya sheria
za usalama barabarani.
Mmoja wa madereva wa mabasi ya wanafunzi Mkoani
Singida Pyuza Gyumi amesema kwenye mafunzo hayo ya muda mfupi wameagizwa kwamba
ni marufuku wanafunzi kuchangia kiti kimoja kwa madai ni ukiukwaji mkubwa
wa sheria za usalama barabarani.
“Tumekumbushwa kwamba wakati tukiwa barabarani tuwe
makini wakati wote wa kuendesha na tuwe na utulivu wa hali ya juu. Pia
tumekumbushwa kuwa makini wakati tunavusha kwa miguu wanafunzi ng’ambo yingine
ya barabara. Kwa ujumla binadamu anatakiwa mara kwa mara akumbushwe wajibu wake
hii itasaidia kufanya kazi zetu kwa ufanisi”, amesema.
Aidha amesema jeshi la polisi kuwakutanisha na
waajiri wao itasaidia kupunguza kero mbalimbali zinazowakabili kati yao na
waajiri wao.
“Kuna wakati tunashindwa kuelewana na matajiri wetu
wakati wanapotulazimisha kutenda mambo ambayo ni nje ya sheria za usalama
barabarani. Baada ya mafunzo haya ya muda mfupi waajiri wenye tabia hizo watabadilika
na kutuunga mkono uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani”, amesema Gyumi.
RTO Mkoa wa Singida Mrakibu wa polisi Peter Raphael Majira akitoa
taarifa ya zoezi la ukaguzi wa mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi kwa
lengo la kukagua ubora na pia kuwakumbusha madereva na wamiliki wa mabasi hayo
juu ya sheria za usalama barabarani.
Picha/taarifa na Nathaniel Limu.
Picha/taarifa na Nathaniel Limu.
No comments:
Post a Comment