Saturday, May 13, 2017

SERIKALI KUAJIRI WATUMISHI WA KADA YA AFYA KUZIBA PENGO LA WALIOONDOLEWA KWA VYETI FEKI.



Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisisitiza jambo katika maadhimisho ya siku ya wauguzi iliyofanyika kitaifa katika hospitali ya St. Gasper Itigi, Mkoani Singida.

Wauguzi kutoka mikoa mbalimbali nchini wakirudia kiapo cha uuguzi katika maadhimisho ya siku ya wauguzi iliyofanyika kitaifa katika hospitali ya St. Gasper Itigi, Mkoani Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwakaribisha wauguzi kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya siku ya wauguzi iliyofanyika kitaifa katika hospitali ya St. Gasper Itigi, Mkoani Singida

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kuajiri watumishi wa idara ya afya ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi ambao wameondolewa katika utumishi wa umma kwa kukosa sifa ya kuwa na vyeti halisi baada ya zoezi la uhakiki wa vyeti nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameyasema hayo jana wakati wa maadhimsho ya Siku ya Wauguzi Duniani ambapo kitaifa imefanyika katika hospitali ya St. Gasper, Itigi Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida.

Waziri Ummy amesema serikali inatambua mzigo mkubwa wa majukumu kutokana na uhaba wa wauguzi ambao umesababishwa na baadhi yao kuondolewa katika utumishi kwa kukosa vyeti halisi na hivyo imetenga bajeti ya kuajiri wauguzi wa kutosha nchini huku akiahidi kutoa kipaumbele kwa mkoa wa Singida.

“Kuna baadhi ya Zahanati na vituo vya afya vimefungwa kwa kutokana na sakata la vyeti feki, lakini pia tunatambua kuwa wauguzi hamtoshi na hivyo kupelekea muuguzi mmoja kutoa huduma kwa wagonjwa wengi, hali hii inapunguza ufanisi wenu na kuwanyima haki ya kupumzika”, ameongeza Waziri Ummy.

Aidha ameagiza waajiri wa utumishi wa umma na hasa halmashauri zote nchini kupeleka maombi ya watumishi wa kada za afya ili wizara iweze kutangaza nafasi hizo zijazwe na watanzania wenye sifa huku akisisitiza kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

 “Serikali imegawa vitanda 25 vya wagonjwa, magoro 25 na mashuka kwa kila halmashauri nchini huku bajeti ya wizara ya afya ikipanda kutoa trilioni 1.9 mwaka jana hadi trilioni 2.2 kwa mwaka wa fedha 2017/18, bajeti hii itasaidia kupambana na changamoto za sekta ya afya nchini nah ii ni ishara kuwa serikali imedhamiria kuimarisha afya za watanzania” amefafanua Waziri Ummy.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Pulo Magesa amewataka wauguzi kuto muangusha waziri wao wa Afya kwa kuwa amekua mstari wa mbele kuhakikisha wauguzi na watumishi wote wa Sekta ya Afya Nchini wanafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha.

Magesa amesema serikali inaweka mazingira mazuri kwa kutenga bajeti ya kutosha ila ufanisi wake utaonekana endapo watumsihi wa sekta ya afya hasa wauguzi ambao ndio muhimili wa vituo vya huduma za afya mfano hospitali, zahanati na vituo vya afya watazingatia misingi ya uadilifu, upendo na weledi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema wauguzi wanaweza kupunguziwa mzigo wa kupata wagonjwa wengi hasa kwa magonjwa yanayozuilika endapo kutaanzishwa mfumo wa utoaji wa huduma za uuguzi kwa ngazi za kaya ambapo kila mwanafamilia atapewa elimu ya kuzuia baadhi ya magonjwa.

Dkt. Nchimbi amesema mfumo huo wa uuguzi kaya uendeshwe mpaka kwenye taasisi za elimu hasa shule za msingi na sekondari ili jamii iweze kuzuia kwa kiwango magonjwa yote yanayozuilika na hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa .

Aidha amemshukuru Waziri Ummy kwa kuunga mkono wazo hilo na kukubali kuanza kulifanyia kazi huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa kuwa mkoa wa Singida utatumika na sehemu ya utafiti wa mfumo huo ili kufahamu ufanisi wake

Maadhimisho Siku ya Wauguzi Duniani ni kukumbuka ya muasisi wa taaluma ya uuguzi Bi.Florence Nightngale aliyezaliwa Mei 12 mwaka 1820. Wakati wa sherehe hizi huwa mishumaa inawashwa kama ishara ya upendo na utumishi bora moyoni mwa muuguzi. Muasisi huyu ndiye aliyefungua chuo cha kwanza cha uuguzi nchini Uingereza.

Bi Florence alianza kutoa huduma ya afya mwaka 1844 na mwaka mmoja baadaye kulitokea vita na yeye akawa anahudumia majeruhi kwa kutumia mishumaa nyakati za usiku kwa vile hapakuwepo na nishati yoyote wakati huo. Bi Florence kwa huduma yake hiyo ya kutibu majeruhi wa vita aliweze kupunza vifo kutoa asilimia 42 hadi asilimia mbili (2).

Wauguzi waliokuwepo kwenye maadhimisho hayo kutoka mikoa mbalimbali nchini walirudia kiapo chao cha uuguzi ambacho sehemu mojawapo inasema “Naapa mbele ya Mungu na mbele ya mhadhara huu, kuendesha maisha yangu na kutekeleza wajibu wangu wa kazi kwa uaminifu. Sitafanya vitendo vyo vyote vile vilivyo viovu na sitochukua au kutoa dawa ye yote ile ninayoifahamu kuwa ina madhara”.

Awali wauguzi, viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya dini pamoja na wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo walisimama kwa dakika moja kuwakumbuka na kuwaombea wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa shule ya Lucy city ya Mjini Arusha waliopoteza maisha yao kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea hivi karibuni.

Wauguzi kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiandamana na kuonyesha ujumbe mbalimbali mbele ya Mgeni rasmi Waziri wa Afya Ummy Mwakimu katika maadhimisho ya siku ya wauguzi iliyofanyika kitaifa katika hospitali ya St. Gasper Itigi, Mkoani Singida.
 
Waziri wa Afya Ummy Mwakimu akisaini zawadi aliyopewa na wenyeji wake halmashauri ya Itigi katika maadhimisho ya siku ya wauguzi iliyofanyika kitaifa katika hospitali ya St. Gasper Itigi, Mkoani Singida.

No comments:

Post a Comment